makubaliano ya madereva na wamiliki magari

VITU VYA KUZINGATIA KWENYE MAKUBALIANO WANAYOINGIA MADEREVA WA TAXI MTANDAO NA WAMILIKI WA MAGARI

Kabla ya kuingia kwenye mkataba wa kukodi gari ni muhimu kufahamu vitu vya kuzingatia kwenye makubaliano wanayoingia madereva na wamiliki wa magari kwa lengo la biashara. Kama unavyofahamu si lazima kuwa na gari lako mwenyewe ili uweze kutengeneza kipato kwa kuendesha abiria wa majukwaa ya usafiri.

Wapo madereva wengi sana ambao wanatengeneza kipato kikubwa tu kwa kukodi magari ya watu na kuingia nao makubaliano kabla ya kukabidhiwa magari na kuanza kazi.

VITU 6 VYA KUZINGATIA KWA MADEREVA NA WAMILIKI MAGARI KABLA YA KUKABIDHIANA GARI

1. KIASI CHA MALIPO

Hili unaweza kusema kuwa ndio la muhimu kuliko yote katika kufanikisha mshikamano kati ya dereva na mmiliki wa gari. Mara nyingi madereva kabla ya kuanza kutafuta gari huwa wanafahamu mahesabu ya kawaida ambayo wamiliki wengi hupendelea.

Kiasi cha malipo ni kile kiasi ambacho dereva anapaswa kumlipa mwenye gari, kama fidia ya kutumia gari lake kwenye biashara ya kuendesha abiria kupitia programu za usafari. Mara nyingi sana madereva wanatakiwa kuwa makini na kufanya utafiti kabla ya kukubaliana na mmiliki kwenye kipengele hiki.

Hii ni kwa sababu mmiliki akitaka kiasi kikubwa kuliko uwezo wa dereva na gharama za uendeshaji, hasara atapata dereva na si yeye. Wamiliki pia wanatakiwa kuwa makini kwasababu wengi wao hawana ujuzi mkubwa kwenye biashara ya udereva kwenye programu za usafiri kwa hiyo ni rahisi kwao kupata hasara kwa kutojua kiasi ambacho magari yao yanaweza kuingiza kwa siku au kwa wiki.

Kiasi cha fedha cha kulipwa mmiliki huwa tofauti kutokana na sababu zifuatazo.

  • Mahusiano ya dereva na mmiliki: kama kuna undugu au urafiki kati ya dereva na mmiliki basi ni rahisi zaidi kwa dereva kuweza kuomba awe analipa kiasi ambacho sio kikubwa sana. Lakini kama hawafahamiani sana basi hii huweza kuwa ngumu kidogo hasa ukizingatia kuwa mmiliki anakuwa kama anajiweka kwenye hatari kwa kumpa mtu asiyemfahamu vizuri gari lake. Lakini hii haimaanishi mahusiano haya ya undungu au urafiki yanaleta tija zaidi kwa wamiliki katika biashara yao ya kukodisha gari kwa madereva wa majukwa ya usafirishaji.
  • Aina ya gari: Wamiliki wa magari ya gharama ndogo ambayo yapo kwa wingi zaidi huwa ni rahisi zaidi kukubali kipato cha chini kuliko wale wenye magari ya bei ya juu zaidi na ya adimu kidogo kwenye majukwaa. Hii Inaweza kuwa ni sawa kwa madereva kama kiasi cha malipo kinaendana na kiasi cha matunzo na gharama nyingine za kuendeshea gari.
  • Hali ya gari: Wamiliki wenye magari ambayo yapo vizuri yaani sio mabovu, au mapya au tu ambayo kila kitu kipo sawa katika uendeshaji na muonekano huweza kuhitaji malipo kiasi kikubwa zaidi ya wale ambayo magari yao yana shida kidogo au ambayo muonekano si mzuri sana.
  • Gharama za uendeshaji: kama gharama ni kubwa kwa mfano mafuta, matengenezo, oil nk. Na faida inakuwa ndogo hasa katika sekta ya usafiri kupitia programu za safari kwa sababu mara nyingi nauli hubaki pale pale. Kwa hiyo mwisho wa siku itabidi hii lizingatiwe ili dereva asiwe tu anapata hasara.

2. MUDA WA MALIPO

Kiasi cha malipo kwa mmiliki huamuliwa pamoja na makubaliano ya muda wa kuwasilisha malipo hayo. Makubaliano haya pia huwa ni tofauti kati ya watu na watu lakini kwa kawaida na kutokana na ripoti za madereva wengi muda unaopendelewa ni malipo ya wiki.

Mmiliki na dereva wanaweza kuamua kuwa dereva anatakiwa kuwasilisha kiasi fulani kila mwisho wa wiki au mwisho wa siku kutegemeana na maamuzi yaliyokubaliwa.

Kutokana na tafiti zetu inaonekana madereva na wamiliki magari wengi hupendelea zaidi malipo ya kila wiki yanayoanzia tsh 150,000 – 180, 000/= kutokana na aina ya gari.

Madereva wengi wanaotuma maombi ya kupata magari kwenye mitandao ya jamii kama Facebook na Jamii forums wanaonekana wakihitaji wamiliki waliopo tayari kwa ajili ya mkataba wa malipo kiasi hiki kwa wiki.

3. MUDA WA MKATABA KATI YA MADEREVA NA WAMILIKI MAGARI

Haya ni makubaliano ya muda ambao gari la mmiliki litakuwa chini ya dereva likitumika kuingiza kipato. Urefu wa mkataba hutegemeana na malengo ya mmiliki pamoja na hali ya gari.

Kwa mfano kama mmiliki anataka kukodisha gari lake kwa muda mfupi tu aliopo kwenye eneo husika basi anaweza kumkabidhi dereva kwa muda huo. Lakini kama mmiliki anaishi eneo husika kwa muda mrefu na hana matumizi mengine na gari lake anaweza kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuandikishana mkataba mrefu zaidi.

Lakini pia kama makubaliano yanahusisha kuhamishwa kwa umiliki wa gari kutoka kwa mmiliki wa gari kwenda kwa dereva pale mkataba utakapofika mwisho. Basi pia mikataba ya aina hii uchukua muda mrefu. Kwa wastani haipungui mwaka na nusu.

Urefu wa mikataba kati ya madereva na wamiliki magari pia hutegemeana na hali ya ubora wa gari wakati wa kuanza makubaliano.

Kwa Magari ya zamani sana huwa madereva hupendelea mikataba mifupi kwa sababu tayari yameshaendeshwa sana na yana uwezekano mkubwa zaidi wa kuharibika muda wowote haraka na kuleta gharama.

Lakini kwa magari mapya au yenye hali nzuri sana yanaweza kuingizwa kwenye mikataba mirefu kwa sababu bado yana nguvu ya kumudu miaka mingi barabani.

Madereva wengi wazoefu wanaonekana kuwa makini sana katika kuulizia na kuhakikisha umri wa magari unaendana na urefu wa mkataba.

Hili ni jambo la kujifunza kwa madereva wapya na pia jambo la kuzingatiwa na wamiliki wa magari kabla ya kuamua kuingia mikataba na madereva.

4. JUKUMU LA GHARAMA YA MATENGENEZO

Gari ni mali ya mmiliki lakini anapokuwa anaendesha dereva nani anapaswa kulipia matengenezo? Hili ni moja ya jambo muhimu sana ambalo hujadiliwa na kukubaliana katika mikataba kati ya madereva na wamiliki wa magari.

Mara nyingi makubaliano kuhusu suala la matengenezo ya gari yanaweza kuwa kama ifuatavyo kutokana na sababu mbali mbali.

  • Mmiliki anaweza kutaka majukumu ya matengenezo yawe juu ya dereva.
  • Mmiliki anaweza kukubali kufanya baadhi ya matengenezo ya kawaida yaani maintanance ile ya baada ya gari kusafiri umbali fulani (kwa mfano kubadilisha oil).
  • Mmiliki anaweza kuamua wagawane jukumu hili.

Kwa kawaida njia inayotumika utegemea zaidi aina ya makubaliano yanayokuwepo kati ya mmiliki wa gari na dereva.

Kama aina ya makubaliano inahusisha uhamishwaji wa umiliki wa gari kutoka kwa mmiliki kwenda kwa dereva pale ambapo mkataba utafika tamati. Basi wamiliki wengi hupendelea kuacha jukumu la matengenezo ya gari kubaki kwa dereva, kwa kuwa kinachofanyika hapa ni kama dereva anauziwa gari kwa malipo ya mara kwa mara kwa kipindi fulani (installment). Lakini pia kwenye makubaliano ya aina hii madereva wengi hukubali kuchukua jukumu la matengenezo kwa kuwa wengi wao huchukulia gari kama mali yao na matunzo huwa mazuri zaidi.

Lakini kama aina ya makubaliano ni ya kawaida yanayohusisha kukodisha gari kwa ajiri ya kujitengenezea kipato tu. Basi madereva wengi pamoja na wamiliki wa magari huchagua zaidi njia mbili zilizobaki.

Kwa kuwa gari kwa wamiliki ni mali inayoweza kuwaingizia kipato endelevu kwa muda mrefu. Basi wamiliki wengi wanaofahamu vizuri biashara yao uamua kuchukua jukumu la matengenezo ya gari. Hii huwasaidia wamiliki wa magari kutunza ubora wa magari yao kwa kuhakikisha kuwa magari yao yanafanyiwa matengenezo kwa njia sahihi, katika sehemu sahihi na kwa wakati sahihi. Hivyo kwenye malipo yao kutoka kwa madereva wamiliki hutenga fungu kwa ajiri ya matengenezo hayo.

Lakini kwa madereva pia njia hii uwasaidia kuepuka gharama nyingi za uendeshaji, kuepuka lawama kutoka kwa wamiliki wa magari na pia kuepuka kufanya kazi inayowafaidisha zaidi wamiliki na wao kukosa faida endapo watabeba jukumu la matengenezo kwenye makubalino ya kawaida.

Ikiwa madereva na wamiliki wakaamua kugawana majukumu ya matengenezo. Basi mara nyingi madereva hubeba majukumu madogo madogo kama vile kujaza upepo, kuziba pancha na kubadilisha oil. Matengenezo makubwa makubwa na ya kawaida katika gari na ambayo hayaja sababishwa na dereva hubaki kwa mmiliki wa gari.

Kwa hiyo dereva anatakiwa kuwa makini na mmiliki pia kuwa makini ili mikataba iwe na usawa na faida kwa wote.

5. MATUMIZI NJE YA KAZI

Ni sahihi kusema kuwa watu wengi wanapokodisha mali zao hupendelea zifanyiwe ile shughuli iliyokubaliwa na si nje ya hapo. Kama mmiliki wa gari na dereva wameazimana gari kwa ajili ya kuendesha kwenye programu za safari tu basi ni kawaida kwa mmiliki kusema kuwa gari lisiendeshwe nje ya shughuli hiyo.

Hii pia husaidia kupunguza uchakavu na lawama kwasababu, pale kosa litakapofanyika au ajali/tatizo litakapotokea wakati gari linatumika nje ya makubaliano ni rahisi kwa adhabu kuwepo kutokana na kukiukwa kwa mkataba.

Wapo wamiliki wengine ambao hawajali dereva anachofanya ilimradi kila wiki analeta pesa kamili iliyokubaliwa.

Lakini wapo pia ambao bado hutaka kuwa na uwezo wa kusimamia mali zao hivyo wakawa wanapendelea kanuni za matumizi.

Kwa mfano, wamiliki wengine hutaka magari yao yaegeshwe majumbani kwao au sehemu wanazoamua wao. Hii ina maana kuwa dereva anakuwa na muda maalumu wa kuanza kazi na kumaliza.

Kwa haraka inaweza kuonekana ni kitu kizuri lakini kwa sekta hii ya usafiri wa kwenye programu za safari kanuni kama hii inaweza kuwa si nzuri kwa dereva.

Hii ni kwasababu majukwaa huwa na wateja muda wowote katika masaa 24. Tena unaweza kukuta siku nyingine usiku wa manane ndiyo kuna abiria zaidi kuliko muda wa masaa ya kawaida ya kazi.

Kwa hiyo kwa madereva wengi wazoefu kupata gari lenye sheria kama hizi za muda na mahala pa kulaza gari ni kama kujiletea hasara kwa sababu wanajua kuwa muda huo wanaoweza kupata gari wanaweza wasipate safari nyingi za kuwafanya wapate hela ya kutosha kumlipa mwenye gari na kujilipa wao wenyewe.

Mara nyingi katika makubaliano ya madereva na wamiliki magari, madereva hupata uhuru mkubwa zaidi wa kuwa na gari hivyo kuwapa uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza kipato kikubwa zaidi.

6. UWAJIBIKAJI KWENYE MAKOSA

Pale gari linapopata ajali nani anatakiwa kulipia fidia au matengenezo?. Kama gari limekatiwa bima sahihi na kampuni ya bima inafahamu kuwa anayeendesha ni mwajiriwa au mkodishwaji na si mmiliki, na kama kosa halikuwa la dereva huyo basi fidia inaweza kuwa si tatizo.

Ni muhimu sana kuchambua uwajibikaji kwenye makosa kwa sababu mtu anapopata ajali na gari husika mara nyingi ni rahisi zaidi kwa wao kumtafuta au kudai fidia kwa mmiliki wa gari hata kama kosa ni la dereva.

Kwa hiyo katika makubaliano kati ya madereva na wamiliki magari ni lazima kipengele hiki kitiwe mkazo ili kulinda pande zote mbili za dereva na mmiliki.

Je umewahi kutumia magari ya kuingia mkataba na wamiliki kuendeshea abiria wa programu za safari?. Mkataba wako ulikuwaje? Tafadhali tushirikishe ili na sisi tuongezee kwenye tafiti zetu.

Pia utakuwa unasaidia madereva wengine waweze kujua hali halisi kabla ya kuingia kwenye upande huu.

Kama haujawahi kupata gari la kukodi kwa ajili ya kuendeshea abiria kwenye majukwaa ya programu za safari, karibu kusoma makala hii ili kujifunza zaidi kabla haujaanza mchakato wa kupata gari.

SOMA: FAIDA ZA DEREVA KUTUMIA GARI LA KUKODI KUENDESHA ABIRIA

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *