Kwanini Uber imesitisha huduma Tanzania

UBER IMESITISHA HUDUMA TANZANIA 2022 KWA SABABU HIZI

Kuanzia tarehe 14 April 2022 kampuni ua Uber imesitisha huduma Tanzania kama ilivyotangazwa na wawakilishi wake. Hili limekuwa jambo la ghafla na ambalo limeathiri kipato cha madereva wengi kwasababu kampuni hii ndio kubwa kuliko kampuni zote za programu za safari Tanzania na dunia nzima.

KANUSHO: Weibak Carsharing sio mdau wa kampuni yoyote ya programu za usafiri. Lengo letu ni kusaidia madereva wa programu hizi kupata taarifa sahihi, kuwaunganisha na kuwaelimisha kuhusu jinsi ya kufanikiwa kwenye sekta hii kwa ujumla.

Kwanini Uber imesitisha huduma Tanzania?

Uber imetaja mazingira magumu ya udhibiti kutoka kwa LATRA kuwa ndicho chanzo kikuu cha kuamua kusitisha huduma nchini. Mnamo tarehe 14 Aprili 2022  mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) ilitoa tamko la kuanza kwa nauli mpya (nauli elekezi) ambapo kampuni ya Uber ilishindwa kukubaliana nayo.

Sababu za kushindwa makubaliano.

1. Kushuka kwa kiwango cha makato

Kama ambavyo tumeshajadili katika makala mbalimbali, Kampuni ya Uber ilikuwa ikiwakata madereva 25% ya nauli kama ada yao ya kutumia jukwaa. Tayari madereva wamekuwa wakilalamikia kiasi hiki kuwa ni kikubwa sana hivyo mamlaka iliamua kukaa na kuamua ishushwe.

Kuanzia 14 April 2022 LATRA iliamua makampuni yote ya programu za safari yakate 15% na si zaidi. Hii imesababisha kampuni ya Uber kuona kwamba faida itakuwa ndogo hivyo kuona ni bora kusitisha huduma.

2. Ukosefu wa uwezo wa kuamua bei

Uber ni kampuni kubwa na kiongozi katika sekta ya usafiri kupitia programu za usafiri. Zaidi ya hapo ni kampuni ambayo inatoka na inaendeshwa na raia wa Marekani. Kampuni nyingi kubwa hupenda uhuru wa kuamua bei za huduma au bidhaa zao.

Kiasi cha 25% ndicho kiasi wanachokatwa madereva Uber dunia nzima. Hichi ndicho kiasi ambacho kwa wao kinawasaidia kuendesha biashara na kuleta faida kwa wawekezaji.

Nchi yoyote inapokuwa na mamlaka inayoamua bei ya huduma katika sekta fulani hupelekea uwezekano wa makampuni kuamua kuacha biashara hasa kama ni makampuni yanayotok nje ya nchi. Tofauti ya 10% inaweza kuonekana ndogo lakini kwa Uber ni punguzo kubwa sana ambalo wameona halifai kwaajili ya biashara.

3. Ukosefu wa sera rafiki katika sekta ya usafiri kupitia programu za safari

Kwa Tanzania usafiri wa programu za safari na huduma ya Taxi za kawaida haujatofautishwa sana. Huduma hizi zinachanganywa kiasi kwamba watu wamezoea kuita huduma hizi “Taxi mtandao” wakati kiutaalamu hazipaswi kuitwa hivi.

Kutokana na hili, sheria au udhibiti unaotumika kwenye usafiri wa taxi hutumika kudhibiti usafiri wa programu za safari hivyo kusababisha matatizo katoka uendeshaji wa makampuni.

Kiukweli huduma hizi mbili ni tofauti kwasababu zina uendeshaji tofauti na hata bei zao na kodi huwa ni tofauti. Kutokana na hili upo uhitaji wa kuwepo sera tofauti maalumu za kuendesha sekta ya ride hailing tu.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo bado inaendelea kuboresha sera na udhibiti sahihi wa sekta hii. Kwa hiyo kwa sasa kampuni hii imeona haitaweza kuendelea kutoa huduma hadi pale mazingira rafiki yatapofikiwa.

4. Kupungua kwa faida

Ingawa kampuni ya Uber ilitangaza kuwa inakata madereva 25% tu, zipo ripoti na tafiti zinazoonesha kuwa madereva hukatwa zaidi ya hiyo. Kutokana na hili, kitendo cha LATRA kushusha kiwango hicho kulihatarisha kushusha mapato ya kampuni ya Uber zaidi ya hata ambavyo inadhaniwa.

Kutokana na taarifa hii Kampuni ya Uber imekuwa ikikata madereva hadi 42.75% kwa kila safari ambapo safari fupi ndio hukatwa kiasi kikubwa zaidi kuliko safari ndefu.

5. Mifumo ya nchi za nje

Kampuni ya Uber imepata changamoto kuendelea kutoa huduma kwasababu imekuwa ikiendesha shughuli katika nchi zinazoendelea (3rd world countries) kama inavyoendesha kwenye nchi zilizoendelea (Marekani).

Kutokana na hili Uber imekuwa ikisitisha huduma katika nchi nyingi hasa za bara Asia. Tofauti za miundo mbinu na hali ya uchumi ya wanananchi ni tofauti kwenye nchi zetu. Hili lilitakiwa kutiliwa maanani hasa katika kupanga makato ya madereva na jinsi ya kukokotoa nauli ya usafiri.

Kutokana na hili, gharama ya huduma imeonekana kuwa kubwa sana kiasi kwamba mamlaka maalumu imebidi kuingilia kati, wakati gharama hizi hizi zinachukuliwa sawa tu katika nchi tajiri.

Yapo mengi mengine ambayo kampuni ingetakiwa kuzingatia kwa ajili ya maslahi ya wadau wa nchi za uchumi wa chini na wa kati kama Tanzania.

Mfano mwingine mkubwa ni uchakavu na matengenezo ya magari. Katika nchi za nje kuna barabara nzuri sana ambazo zinafaa sana kwa magari ya aina yote. Lakini huku kwetu zipo barabara nyingi ambazo hazikidhi viwango na zinaleta tu athari kubwa kwa vyombo vya usafiri.

Hivyo madereva wa huku hujikuta wakiiingia gharama za matengenezo mara kwa mara ukilinganisha na wa nchi zilizoendelea. Pia hujikuta vyombo vyao vikichakaa kirahisi kutokana na kuvitumia mara kwa mara kwenye barabara mbovu.

Kutokana na utofauti huu ni dhahiri kwamba madereva wa nchi yetu hawakutakiwa kuwa wanakatwa asilimia kubwa ya 25.

Je, ina maana kuwa Uber imesitisha huduma Tanzania milele?

Kutokana na taarifa maalumu iliyotolewa, kampuni imesema kuwa imesitisha huduma kwa muda hadi itakapofikia muafaka rafiki zaidi na LATRA.

Kampuni ya Uber imenukuliwa kusema kuwa “Tumefanya uamuzi mgumu wa kusimamisha huduma zetu nchini Tanzania kuanzia Alhamisi tarehe 14 Aprili 2022. Nauli elekezi iliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) imeleta changamoto kubwa kwa mifumo ya Uber kuendelea kutoa huduma kwa wateja wetu. Hatutaweza kutoa huduma hadi mazingira yawe rafiki kwa kuendelea kutoa huduma,”

Iliendelea pia kusema “Tulitarajia kwamba tamko hili lingejumuisha kuweka mazingira wezeshi kwa biashara za ndani na za kimataifa kustawi kwa njia chanya na yenye uwiano, lakini kwa bahati mbaya, hali ni kinyume na matarajio,”. Lakini juu ya yote kampuni imesema kuwa itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na mamlaka husika ili kufikia makubaliano ambayo yataleta uwiano kwa ajili ya biashara.

Habari nzuri ni kwamba kama ambavyo tayari unafahamu, zipo kampuni nyingine nyingi za programu za usafiri Tanzania. Zaidi ya hapo kampuni hizi zina mwamko wa kuchukua soko ambalo Uber imeliacha nyuma baada ya kusitisha huduma.

SOMA HAPA: Kufahamu hatua za kuchukua kama kusitishwa huduma kwa kampuni hii kumeyumbisha uchumi wako kidogo. Hapa utaona njia nyingine za kufanya ili kuziba pengo la kipato ambalo hatua hii ya Uber imesababisha.

Je mtazamo wako ni upi mdau?

Unadhani kampuni ya Uber itarudisha huduma zake Tanzania au itasitisha milele?

Tafadhali tushirikishe mtazamo wako kwenye sehemu ya comments ili sisi pamoja na madereva wengine tuweze kupata kitu kutoka kwako.

Usisahau kuendelea kutembelea Weibak website pamoja na kurasa zetu za mitandao ya jamii ili kuendelea kupata habari na ujuzi mwengine wa biashara hii ya usafiri wa kupitia programu za safari.

3 thoughts on “UBER IMESITISHA HUDUMA TANZANIA 2022 KWA SABABU HIZI”

  1. SERAPHIN KESSY

    Jaman naona mm kama dreva wa tax mtandao bora Uber ilikuwa vizuri sana kwenye maswala ya bei.ila hata wakirudi washushe asilimia hata ikiwa 20% tutafanya kazi.hizi App nyingine ni wazinguaji tu.uber naikubali sana.je wanarudisha huduma lini?

    1. Seraphin, Tunashukuru sana kwa maoni yako kuhusu ubora wa huduma za Uber kwako kama dereva.

      Endelea kufuatilia makala zetu, iliupate taarifa mara tu Uber watakapo rudisha huduma zao.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *