Taxi na programu za safari ni tofauti

TOFAUTI 9 KATI YA TAXI NA PROGRAMU ZA SAFARI

Mara nyingi sana watu hufikiria kuwa teksi na programu za safari kama Bolt, Linkee, moovn nk ni kitu kile kile. Lakini ukweli ni kwamba Taxi na programu za safari ni huduma mbili tofauti ambazo zinapaswa kutochanganywa kabisa.

Huduma hizi ni tofauti kwasababu kuna utofauti mkubwa katika muundo wake wa biashara na mfumo wa utoaji huduma.

Tofauti kati ya Taxi na Programu za safari

1. Usajili

Ili kusajili kupata leseni ya taxi mmiliki anatakiwa kutembelea ofizi za halmashauri ya wilaya yake pamoja na nyaraka zifuatazo;-

  • Kadi halisi ya chombo
  • Sticker ya mapato toka TRA
  • Taxi cab
  • Taarifa ya ukaguzi toka kwa mkaguzi wa vyombo vya moto (V.I.R)
  • Barua kutoka kwenye kituo ambacho mwombaji anataka kwenda kufanyia kazi
  • Gari liwe jeupe
  • Ada ya usajili Tshs 20,000/=

Madereva wa programu za safari hawalazimiki kuwa na leseni za taxi wala kuweka alama za taxi cab kwnye magari yao. Wao hutuma maombi kwa kampuni ya programu ya safari yakiambatanishwa na nyaraka kama zifuatazo:

  • Leseni ya dereva
  • Kadi ya chombo
  • Bima ya biashara
  • Passport size photo

2. Upatikanaji

Madereva wa taxi za kawaida mara nyingi hupata wateja kwa kuwasubiria wawafate au wawasimamishe wakiwa barabarani hawana abiria.

Zamani ilikuwa abiria akifika kwenye kituo cha taxi madereva wanaanza kumgombania hadi kufikia hatua ya kukosana.

Baada ya muda utaratibu bora zaidi ulianzishwa ambapoTaxi huwa zinapanga foleni, hivyo kusababishwa utulivu na usawa kwa kila dereva. Abiria mpya anapofika kituoni huwa mara nyingi hachagui yeye gari bali Taxi lililopo mbele kabisa kwenye foleni humpatia huduma.

Hii ni tofauti kabisa na programu za safari ambapo abiria hutumia programu za majukwaa ya usafiri (App ya simu janja) kuitisha gari. Mara nyingi pia abiria hana shida ya kufata gari kwenye kituo. Badala yake dereva anamfata yeye hivyo kuongeza kwa ubora wa huduma.

Kwa hiyo katika pointi hii upatikanaji wa abiria kwa madereva na upatikanaji wa dereva kwa abiria ni tofauti kutokana na matumizi ya teknolojia.

3. Uhakika wa usafiri

Kwa taxi za kawaida abiria anaweza kufika kituoni na akakosa kabisa usafiri hasa kwenye masaa ambayo abiria ni wengi sana.

Katika upande wa programu za safari, madereva wapo wengi sana hivyo kukosa usafiri ni kitu adimu sana!. Madereva taxi pia hupenda kuwapa namba zao za simu wateja wao ili wawatafute wanapohitaji usafiri. Lakini hata katika hili uhakika pia sio mkubwa kwasababu dereva anaweza kuwa na abiria mwingine au awe amepumzika.

Huduma za programu za safari ni kama zinampa abiria uwezo wa kupata huduma kutoka kwa kwa mamia ya madereva bila kuhitaji kuwasiliana nao binafsi.

3. Usalama

Huduma za programu za safari zinadhibitiwa sana na makampuni husika hivyo usalama upo wa hali ya juu kwa abiria na dereva.

Hii ni kwasababu makampuni haya hutumia nyenzo mbali mbali za kiteknolojia kama GPS kujua eneo magari yote yalipo. Pia huwa na huduma zaidi za usalama kama kurahisisha mawasiliano kati ya dereva/abiria na vituo vya polisi na makampuni ya ulinzi.

Tafiti zinaonesha kuwa hata usalama wa mizigo kwenye magari ya programu za safari ni mkubwa sana kuliko kwenye taxi za kawaida. Kwenye tafiti hii iliyofanyika Tanzania imeonekana kuwa 82% ya abiria waliowahi kupoteza vitu vyao kwenye teksi hawakuweza kuvipata tena.

Hii ni kwasababu teksi za kawaida hazina mfumo wa kufatilia safari (tracking) kama kwenye programu za safari.

Abiria pia huwa na amani kwenye usafiri wa programu za safari kwasababu taarifa zote za dereva zinaonekana na safari zote huwa zinarekodiwa kwa hiyo si rahisi kupelekwa eneo ambalo sio lengo la safari.

4. Bei

Gharama za nauli za kwenye programu za usafiri ni tofauti kuliko gharama za taxi. Zipo sababu mbali mbali zinazopelekea hili lakini ya muhimu ni kwamba programu za safari hutumia teknolojia kukokotoa nauli ndogo zaidi kwa kuchagua njia fupi zaidi.

Katika tafiti hii washiriki 86.4% walisema kuwa wakipanda taxi za kawaida huwa wanalipa zaidi ya vile wakitumia usafiri wa programu za safari kwa kuelekea eneo lile lile.

Hii haimaanishi kuwa madereva taxi wanafanya vibaya kutoza nauli kubwa. Wao hawapati abiria kwa urahisi kama madereva wa programu za safari wanavyopata.

Pia wengi wao hawana teknolojia ya kuwaonesha njia nzuri zaidi na hali ya barabarani. Kwa hiyo lazima kuzingatia mambo kama haya katika kuamua bei.

5. Sheria na muonekano

Taxi zote ni lazima ziwe na muonekano mmoja ambao ni gari jeupe lenye stika ya taxi na namba ya taxi pamoja na alama ya taxi juu ya gari.

Kwa upande wa programu za safari hakuna sheria ya rangi za gari na nembo sio lazima kwasababu gari moja linaweza kuwa limesajiliwa kwenye makampuni zaidi ya moja.

Taxi pia zinatakiwa kuwa na mstari wa rangi ya manispaa inayofanyia shughuli na kupaki kusubiri wateja. Magari ya programu za usafiri hayana udhibiti wowote wa kusafirisha wateja.

6. Kipaumbele / nguvu kwa abiria vs dereva

Katika programu za safari abiria husikilizwa zaidi na pia wanaweza kuharibu uwezekano wa dereva kupata wateja wengine mbeleni.

Hii ni kwasababu huduma hizi huwa na mfumo wa kutoa alama (Star reviews) ambapo kama abiria amevutiwa na huduma huweza kumpa dereva alama za juu. Lakini kama hawajafurahishwa wanaweza kuwapa madereva alama mbaya hivyo kupelekea kuweka fursa zao matatani.

Katika Taxi za kawaida ni ngumu kwa abiria kuharibu kazi ya dereva kutokana na mapishano tu.

Kingine madereva wa programu za safari huweza kupoteza uwezo wa kupata abiria kutokana na kufungiwa akaunti (kihalali au bila kustahili) au matatizo ya kitaalamu ya jukwaa (zinapokuwa zimepata hitilafu au kudukuliwa).

Kwa hiyo katika hili Taxi huonekana kuwa na usalama mkubwa zaidi wa ajira kwa madereva kuliko programu za safari.

7. Uongozi na udhibiti

Ukiachana na LATRA, shughuli za usafiri wa programu za safari huendeshwa na makampuni yanayomiliki majukwaa husika. Hii inamaanisha kuwa kuna ngazi mbili za udhibiti ambazo zina faida na hasara zake kwa madereva.

Madereva wa programu za usafiri huwa na sheria nyingi sana ambazo wanatakiwa kuzifata ili kuweza kuendelea kutumia jukwaa fulani kusafirisha abiria. Madereva Taxi za kawaida wapo huru zaidi kwasababu hawategemei kampuni yoyote kupata wateja.

SOMA: Sheria za Latra kwa makampuni na madereva wa programu za mtandaoni.

8. Njia za malipo

Mara nyingi zaidi madereva taxi hupendelea kulipwa kwa fedha taslimu. Hii ndio njia ya haraka na salama kwao kwasababu biashara hii haitolewi kwa kutegemea hatua zozote za kidijitali.

Kwa upande wa programu za safari zipo njia tofauti za kulipia huduma. Lakini inayoshauriwa zaidi ni kulipa kielektroniki. Hii ni kwasababu inakuwa rahisi kwa wamiliki jukwaa kuweza kukata ada yao ya 15% kabla ya kumuwekea dereva fedha kwenye akaunti yake.

Katika usafiri wa taxi kama dereva ndio mmiliki basi hana shida ya kugawana nauli aliyopata na mtu yeyote. Kama dereva ameajiriwa na mmiliki wa taxi basi huwa na makubaliano ya kulipa kwa siku, wiki au mwezi.

Madereva wa programu za safari ambao ndio wamiliki wa magari huwa wanakatwa mara moja tu na kampuni. Lakini kwa wale ambao wamepewa gari waendeshe, hawa ni kama wanakatwa mara mbili kwasababu ya kugawana faida na mwenye gari.

9. Ukaribu na waleta mabadiliko

Kama tulivyosema hapo awali, taxi za kawaida zinadhibitiwa na mamlaka iliyopo nchini. Kutokana na hili ni rahisi zaidi kwa watoa huduma hawa kupata jukwaa la kusikilizwa na kufanya maombi yao na mabadiliko kufanyiwa kazi mapema zaidi.

Katika upande wa programu za safari kwanza kabisa wamiliki wengi wa makampuni wanatoka nje ya nchi. Hii inafanya mlolongo wa kusikilizwa na kuleta mabadiliko muhimu kuwa mrefu sana kwasababu ya ngazi za uongozi, sheria tofauti za uendeshaji na umbali wa viongozi.

Je umewahi kuwa dereva Taxi na dereva programu za safari? Tofauti kubwa ulizozigundua ni zipi? Na ipi unaipenda zaidi?

Tushirikishe kwenye comments ili na sisi tujue!

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *