akaunti ya dereva uber imefungwa

SABABU ZA KUFUNGIWA AKAUNTI YA DEREVA UBER

Moja ya kero kubwa inayowapata madereva Uber ni kufungiwa akaunti. Mara nyingi madereva wengi hujikuta kwenye balaa hili bila kujua sababu za kufungiwa akaunti zao, hivyo kuishia kupoteza kipato na muda mwingi kwa kujaribu kutafuta suluhusho.

Kwanini kufungiwa akaunti kunaudhi madereva?

  1. KUTOKUWA NA TAHADHARI: Wapo madereva wengi ambao wamejikuta akaunti zao zikifungwa ghafla bila taarifa na kubaki wanashangaa kosa ni lipi. Ni vizuri kama kampuni ingekuwa inatoa muda mfupi wa tahadhari hasa kwa yale makosa ambayo si ya kudhuru abiria. ujumbe wa tahadhari mara nyingi hutumwa pale ambapo dereva anaenda kufungiwa akaunti kwasababu ya kuwa na alama za nyota za chini sana.
  2. KUPOTEZA MUDA: Wa kutengeneza pesa na pia muda utakaoenda kutumika katika kufuatilia akaunti kufunguliwa tena. Kama ambavyo tayari tumesema mara nyingi katika blog yetu, upo ugumu kidogo katika kupata mawasiliano na uongozi wa Uber au wahudumu wa customer care kuliko kwenye makampuni mengine kama Bolt. Kwa hiyo pale dereva anapofungiwa akaunti ghafla kuna uwezekano mkubwa sana wa yeye kutumia muda mrefu kupata suluhisho.
  3. KUONEWA: Madereva wengi hufungiwa akaunti bila hatia lakini bado hulazimika kupoteza muda na kipato hata kama baadaye watagundulika kuwa kweli hawakustahili kufungiwa akaunti.

SABABU ZA KUFUNGIWA AKAUNTI YA DEREVA UBER

1. Kwenda kinyume na sheria za jumuiya

Uber ina sheria ambazo ni lazima kwa madereva wote kuziheshimu na kuzizingatia muda wote. Sheria hizi (community guidelines) ambazo zimeorodheshwa kwa undani kwenye website ya Uber zina lengo la kujenga jamii ya wadau yenye usalama, kuheshimiana na mtazamo chanya.

Tumeweza kuzidadavua sheria hizi kwa lugha rahisi inayoeleweka na kwa kiswahili katika makala hii ya sheria za utoaji huduma Uber. Itakuwa vizuri kama utaweza kutembelea na kujikumbusha mara baada ya kumaliza makala hii.

2. Nyota kushuka

Kila dereva mpya wa Uber anapoanza kuendesha abiria hupewa alama ya nyota 5 na kampuni automatically. Sheria iliyopo nikwamba hairuhusiwi kwa dereva kuwa na chini ya nyota 4.6 kwasababu Uber inataka madereva bora tu watoe huduma kwenye jukwaa lao.

Abiria ndio humpa dereva alama ya nyota kwa hiyo kushuka kunaweza kuwa kwa haki kweli au kunaweza kuwa tu kwa bahati mbaya ya kukutana na abiria ambao sio wema.

Alama yako ya nyota inaposhuka sana hadi kukaribia kile kima cha chini, utapata ujumbe mfupi au email kutoka Uber inayokutahadharisha kuwa alama yako ipo chini sana na unakaribia kufungiwa akaunti.

3. Nyaraka kupitwa na wakati

Dereva anapojisajili Uber hulazimika kupakua nyaraka kama leseni ya udereva, bima nk. Nyaraka hizi huwa zina muda maalumu wa kudumu na muda wa kuisha.

Mitambo ya Uber inatunza taarifa zote za madereva kwa kutumia system za kisasa. Kutokana na hili, ni rahisi kwao kugundua madereva ambao nyaraka zao zimepitwa na wakati na kufunga akaunti zao.

4. Nyaraka zisizo sahihi

Ikijulikana kama dereva amewasilisha nyaraka ambazo sio zake au fake basi akaunti yake hufungwa mara moja. Kampuni ya Uber ina njia mbali mbali za kukagua nyaraka. Kwa mfano huwa madereva wanaweza kutumiwa ujumbe muda wowote unaowaambia wajipige picha na kuipakua kwenye app ili mitambo ya Uber iweze kuhakiki kama mwenye nyaraka ndiye anayeendesha.

5. Ubaguzi

Kampuni ya Uber ina sheria kali juu ya ubaguzi. Ikitokea abiria akalalamika kuwa umembagua kutokana na jinsia, dini, kabila au ulemavu huwa wanafunga akaunti mara moja kwasababu wao huichukulia hili kama unyanyasaji.

6. Kuuza akaunti

Wapo watu wengi ambao kwasababu wana vigezo na nyaraka kamili huwa wanajisajili kama dereva kisha kuwapa watu wengine au kuwauzia akaunti waendeshe na wagawane faida.

Uber wakigundua hili akaunti hufungwa mara moja na kuirudisha kwake inakuwa mtihani mkubwa.

7. Uhalifu

Inapotokea dereva amepata shutuma za uhalifu aidha kutoka kwa abiria au kutoka kwa polisi basi akaunti lazima ifungwe. Kampuni ya Uber ina sheria kali kuhusu wahallifu, ndio maana kabla ya kukubaliwa kuendesha Uber ni lazima waombaji wawe na cheti cha tabia njema kutoka polisi.

8. Silaha kwenye gari

Inapotokea ripoti kuwa dereva ana aina yoyote ya silaha kwenye gari hata kama ya kujilinda mwenyewe mara nyingi akaunti hufungwa. Baada ya hapo dereva anapaswa kuwasiliana na uongozi ili kuhakikisha kuwa silaha ameitoa na hataiweka tena.

9. Utovu wa nidhamu na fujo

Kampuni ya Uber husisitiza sana madereva kutoa huduma kwa heshima na ustaarabu. Endapo abiria watatoa malalamiko ya kukosewa heshima au kufanyiwa fujo kama kupigwa pale wanapopishana na kauli na dereva, hatua ya kwanza kabisa ambayo kampuni itachukua ni kufunga akaunti ya dereva.

Hii ni kwasababu kampuni inajali wateja wake sana na inafanya juu chini kuepuka kesi za kudaiwa fidia.

10. Vilevi kwenye gari

Ikijulikana kuwa dereva anatumia vilevi kama pombe, madawa ya kulevya ya vingine vya kuvuta kwenye gari au wakati anapokea abiria na kuwasafirisha basi ni lazima akaunti ifungwe mara moja.

Mara nyingi abiria huwa makini sana na madereva na huwa wepesi kutoa taarifa kwasababu na wao wanajali usalama wao.

11. Ku cancel safari sana

Madereva Uber wanaruhusiwa kucancel safari ndio. Lakini pale ambapo kiasi cha kucancel kinapokaribia na kuzidi kipimo cha safari zilizokamilishwa basi kampuni huchukulia kwamba dereva aidha haiwezi kazi, au hayupo serious na kuifanya kwa ufanisi.

Inapotokea hali hii kampuni huamua kufunga akaunti ya dereva ili kuwapunguzia kero abiria. Pili kuwapa nafasi madereva wengine ambao wapo serious waweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.

12. Kutokuwa online kwa muda mrefu (siku 90)

Wapo watu ambao hujiunga kama dereva lakini baada ya muda wa kuona kama biashara haiendi huacha shughuli kwa muda mrefu. Hii inaweza kutokea pia kama dereva aliumwa akashindwa kuendelea na kazi au pale ambapo alipata safari hivyo kusitisha kazi.

Jukwaa la Uber linatumia teknolojia ya hali ya juu kuendesha shughuli zake za kila siku. Akaunti za madereva ambazo hazitumiki zinakuwa zinaongeza mzigo kwenye uwanja huu hivyo inakuwa na manufaa zaidi kuziondoa na kuweka nafasi wazi kwa ajili ya madereva wapya kufungua akaunti.

13. Kusambaza picha/video za abiria

Madereva wengi hushauriwa kuwa na camera ya kurekodi wakati safari inaanza hadi inaisha. Hii husaidia sana katika kuwepo kithibitisho pale ambapo dereva anaweza kuwa ameonewa na abiria kama kusingiziwa kuwa amemnyanyasa.

Lakini wapo madereva ambao badala ya kufuta zile video baada ya muda kama hakuna malalamiko yoyote, huwa wanaweza kutumia zile video kupost kwenye mitandao au kwa watu tu wanaofahamiana nao kutokana na sababu moja au nyingine.

Hii inaenda kinyume na sheria za Uber na ikigundulika kama dereva amefanya hivi basi akaunti yake lazima ifungwe hadi atakapowasilisha utetezi wake.

14. Hacking / udukuaji

Hii ni njia ya kutumia mbinu mbalimbali za kiteknolojia kuilaghai mitambo au teknolojia ya jukwaa la Uber. Mara nyingi watu wenye elimu ya kudukua wanaweza ku hack akaunti za madereva , kuwanyang’anya na kuzitumia wao.

Jukwaa la Uber lina uwezo wa kutambua hili na kufunga akaunti hizo mara moja. Mara nyingi hili linapotokea madereva huwa hawana msaada kwasababu linakuwa si kosa lao. Hivyo hupata kero ya kuanza kufatilia na kuhakikishia Uber kuwa sio wao waliohack.

15. Utapeli

Ikigundulika kuwa dereva anachukua hatua zozote kufanya safari ya abiria iwe ndefu sana na kumsababishia gharama kubwa zaidi basi akaunti yake inaweza kufungwa.

Hii ni kwasababu wapo madereva wengi wanaosafirisha abiria kwenye bara bara zile zile. Ikionekana wewe tu ndio unachelewa sana mara kwa mara wakati wenzako wanaenda kwa muda sahihi basi watajua unafanya makusudi ili gharama iwe kubwa.

Kama vile ipo sababu nyingine ya kuchelewa mfano hitilafu ya gari , itakuwa ni rahisi kurudisha akaunti yako hasa kama unavyo vithibitisho.

Je umewahi kufungiwa akaunti yako ya Uber? Unakubaliana na hizi sababu za kufungiwa akaunti au kuna nyingine hatujajadili? Kama umewahi kufungiwa, je sababu za kufungiwa akaunti yako zilikuwa ni zipi?

Kwenye makala ijayo tutaenda kuchambua jinsi ya kurudisha akaunti yako iliyofungwa na jinsi ya kuzuia kufungiwa tena. Kwa hiyo ni vizuri kama utajisajili kupata taarifa makala itakapo kuwa hewani.

1 thought on “SABABU ZA KUFUNGIWA AKAUNTI YA DEREVA UBER”

  1. Pingback: FUNGUA AKAUNTI YA UBER ILIYOFUNGWA KWA KUFATA NJIA HIZI

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *