Kutokana na ripoti zilizopo, madereva huweza kutengeneza pesa zaidi kwa kuendesha abiria maeneo yenye ongezeko la nauli katika jukwaa la Uber.
Ongezeko hili linalofahamika kama surge pricing lililoanzishwa na kampuni hii mwaka 2014 hutokea pale ambapo kwenye eneo fulani kuna abiria wengi kuliko madereva.
Inapotokea hii, algorithm au mitambo ya Uber automatically hupandisha bei za safari ili kuvutia madereva walio nje ya eneo lile waende kufata nauli kubwa hivyo kuepusha abiria kusubiri sana.
Uber ilianzisha system hii kwa ajili ya abiria wao. Wengi walikuwa wanalalamika na kuandika review mbaya kwasababu walikuwa wanasuburi muda mrefu sana kupata Uber. Pia madereva walikuwa hawapendi kwenda umbali mrefu kufata abiria, hivyo ili kuwatamanisha wakaamua kupandisha nauli pale ambapo kuna uhaba wa huduma.
ONGEZEKO LA NAULI HUTOKEA WAKATI GANI?
Wakati wowote ambapo kuna eneo ambalo abiria ni wengi kuliko madereva nauli huongezeka. Hii huweza kutokea kutokana na mambo yafuatayo:
- Matamasha, mechi za michezo au mikutano mikubwa: Muda karibia na kuanza pamoja na kuhitimishwa kwa matukio haya huwa kuna watu wengi sana ambao wanaweza kushindwa kutosha kwenye usafiri wa kawaida wa daladala. Hii ni kwasababu matukio haya huisha muda ambao daladala nyingi zinakuwa zimemaliza kazi.
- Mvua kubwa: Kipindi hiki ni kigumu sana kwa watu wasiokuwa na usafiri binafsi. Wengi hawapendi kulowa na daladala huwa yanajaa sana. Hii husababisha wengi kupendelea usafiri wa ride hailing ili kuhakikisha hawalowi, hawachafuki na hawapati kero wakati wanapoelekea kwenye shughuli zao.
- Kumbi za starehe: Zipo nyumba za starehe ambazo zina muda maalumu wa kufunga. Muda huu kunakuwa na watu wengi ambao aidha wanaamua kurudi nyumbani au kuhamia kwenye sehemu nyingine ambayo ina huduma nzuri zaidi.
Wakati wa usiku mara nyingi ongezeko la bei hutokea kwenye mida ya saa nane usiku kwasababu nyumba nyingi za starehe zinaanza kufungwa au watu huanza kwenda kwenye sehemu nyingine nzuri zaidi.
ONGEZEKO LA NAULI HUKAA KWA MUDA GANI?
Kama ambavyo tumejadili, ongezeko la bei hutokea pale abiria wengi wanapo request usafiri sehemu ambayo madereva wapo wachache.
Mara baada ya madereva kusogea sehemu husika na kuchukua abiria bei hurudi kwenye kima kile kile cha zamani.
Kwa hiyo hakuna kipimo maalumu cha kujua ongezeko litakuwepo kwa dakika ngapi mara baada ya kuanza. Lakini kwa kawaida kama eneo halipo karibia na barabara yenye foleni kubwa basi ongezeko huweza kukaa kwa wastani kama dakika tano hadi nusu saa.
Muda huwa ni mchache kwasababu wale madereva walio karibu na eneo lenye ongezeko wote huharakisha kule. Hii hupelekea app ijue kwamba sasa madereva wengi wapo karibu na abiria hivyo kurudisha nauli kama ilivyokuwa mwanzo.
ONGEZEKO LA BEI YA NAULI LINA FAIDA KWA MADEREVA?
Kwasabau dereva hupata nafasi ya kutengeneza nauli zaidi kwa umbali ule ule, ongezeko la bei lina faida kubwa kwa madereva wanaowahi.
Huu ndio wakati pekee ambapo inaonekana kama Uber inafaidisha madereva zaidi kuliko abiria kwasababu abiria wanapata hasara ya kulipa nauli zaidi.
DEREVA ANATAMBUAJE KAMA KUNA ONGEZEKO LA NAULI SEHEMU FULANI?
Kwenye app ya dereva, maeneo yenye ongezeko la nauli (Price surge) hubadilika na kuwa na rangi nyekundu. Pia Uber huweza kuonesha nauli imeongezeka kwa kiasi gani kwa kuweka namba 2X, 3X au 4X kwenye maeneo mekundu kuashiria nauli imezidi mara ngapi ile nauli ya kawaida.
JE, UENDE ENEO LENYE ONGEZEKO LA NAULI?
Ingawa maeneo haya yana faida zaidi kwa muda huo, sio kila wakati inafaa kwenda kufata ongezeko. Hii ni kwasababu kama tulivyosema, ongezeko la nauli linakuwepo kwa muda mchache tu.
Upo uwezekano mkubwa wa wewe kuamua kwenda na kabla ya kufika ongezeko liwe limeisha hivyo kupelekea kupoteza mafuta tu.
FATA ONGEZEKO LA NAULI KAMA:
- UMBALI MFUPI: Kama eneo lenye ongezeko la nauli lipo karibu yako yaani sio zaidi ya umbali wa dakika 10 basi unaweza kuwahi fursa. Hii ni kwasababu ongezeko huwa linakuwepo kwa muda mfupi tu. Pia mara nyingi sana madereva wengi hukimbilia huko, kwa hiyo kama wewe upo mbali kuna uwezekano mkubwa wa kupitwa nao.
- ONGEZEKO KUBWA: Kama nauli imepanda sana hasa zaidi ya 10,000/=tsh na wewe haupo mbali basi ni vizuri kujaribu bahati yako kwasababu unaweza pata abiria anaayeenda masafa marefu hivyo kupata kipato kikubwa zaidi.
- MUDA WA KUMBI ZA STAREHE KUFUNGWA: Kama tayari unafahamu kuwa sehemu fulani maarufu huwa zinafungwa muda fulani ni vizuri kujaribu kwenda. Hii ni kwasababu unakuwa na uhakika zaidi kuwa watu huwa wanaendelea kuondoka eneo lile hadi kwenye mida fulani hivyo unaweza hata kuwahi ongezeko kabla halijaanza.
USIFATE ONGEZEKO KAMA
- UMBALI NA FOLENI: Kama unajua kabisa kuwa barabara za kufika eneo husika huwa zinakuwa na foleni sana basi ni bora kutokwenda. Madereva walio karibu zaidi hakika watafika pale kabla yako wewe wakati ukiwa bado kwenye foleni.
- ONGEZEKO DOGO: Kama nauli imepanda kidogo tu ni bora kutofuata eneo hilo. Hii ni kwasababu gari linatumia mafuta ambayo gharama yake inabidi izingatiwe katika kutengeneza faida. Unaweza kukuta ongezeko dogo, muda uliotumia barabarani pamoja na mafuta vikawa na gharama zaidi hivyo kukupa tu hasara. (SOMA HAPA JINSI YA KUOKOA GHARAMA YA MAFUTA)
- KAMA KUNA ABIRIA MAHALA ULIPO: Kubali request za safari hapo ulipo hata kama nauli ndogo kuliko ya kwenye ongezeko. Hii ni kwasababu hapo una uhakika wa kupata safari. Huko kwenye ongezeko unaweza kufika na ukakosa. Hivyo mara nyingi kama kuna abiria ulipo au karibu zaidi, mchukue huyo badala ya kufata ongezeko.
Kama tayari upo kwenye eneo maarufu halafu eneo la karibu kukawa na ongezeko la nauli pia ni vizuri kubaki pale pale. Ndani ya muda mfupi madereva wengi watatoka hapo kufata ongezeko huku wakisababisha upungufu wa madereva hapo ulipobaki.
Kama kweli hilo ni eneo lenye abiria wengi basi hili likitokea, wakati abiria watakapoongezeka wewe tayari utajikuta upo kwenye eneo linalongezwa bei.
Lingine la kufahamu ni kwamba abiria hawapendi kabisa hili suala la ongezeko kwasababu wao wanalipa zaidi kwa umbali ule ule. Hivyo unaweza kukuta abiria amekwazika sana na akaishia kukupa lawama au kukupa wakati mgumu kwasababu wanaona kama ni wewe umeongeza bei wakati ni kampuni.
Kuwa mvumilivu na jitahidi kuwaelekeza kuwa ni mfumo tu wa kuhakikisha wao wanapata usafiri maana, bila ya ongezeko madereva wasingesogea hapo na wao ingewabidi kutafuta njia nyingine ya usafiri.
Je, umewahi kupata safari kwenye eneo lenye ongezeko la nauli?. Ulipata ongezeko la kiasi gani?
Karibu kutoa mchango wako kwenye sehemu ya comments ili madereva wengine pamoja na sisi tuweze kujifunza kutoka kwako!