mbinu za usalama kwa madereva usiku

MBINU ZA USALAMA KWA MADEREVA WANAOENDESHA USIKU

Kila dereva anayetoa huduma kwenye majukwaa ya usafirishaji anapaswa kufahamu mbinu za usalama wakati wa kuendesha abiria usiku.

Madereva waliopo nje ya Tanzania au bara la Afrika mara nyingi hawapo katika hatari sana usiku kulinganisha na madereva wa huku kwasababu nchi zao zina miundombinu mikubwa sana ya usalama.

Katika nchi yetu ambayo hata namba ya simu ya polisi kama 911 ya Marekani ni kitendawili, ni muhimu madereva wa kwenye majukwaa ya usafiri kama Uber, Bolt, Lyft, Linkee nk wawe makini sana kujiepusha na majanga.

Mbinu za usalama kwa madereva wanaoendesha usiku

1. FUNGA MILANGO WAKATI WOTE

Muda wowote hasa wakati gari halitembei hakikisha kila mlango umefungwa. Zipo simulizi nyingi mtandaoni ambapo madereva wamekuta watu wakiingia kwenye magari yao bila hata ruhusa kwa lengo la kuwaibia, kwa bahati mbaya au kuwalazimisha wawasafirishe.

Hasa kama upo eneo ambalo hakuna madereva wengi ni rahisi watu kuingia kwenye gari wakikuta lipo wazi. Baada ya hapo itakuwa kazi nyingine kubwa kuwatoa bila kupishana kauli.

2. KUWA MAKINI NA MAGARI BARABARANI

Hata kama uwe dereva mzuri kiasi gani hauwezi kuzuia kupata ajali hasa wakati wa usiku. Hii ni kwasababu madereva wengi katika muda huu hukumbwa na changamoto zifuatazo:

  • Ni ngumu kuona vizuri wakati taa za magari mengine zikikumulika usoni.
  • Barabara ikiwa wazi watu wengi huendesha magari yao kwa fujo sana.
  • Watu wengi hunywa pombe na kuendesha hovyo wakiwa wanarudi nyumbani.
  • Waendeshaji wengi (hata wewe) wanaweza kuwa wamechoka hivyo kuendesha huku wakisinzia.

Kwasababu hii ni muhimu sana kuwa makini ukiwa barabarani. Kama umechoka sana ni bora kurudi nyumbani na kupumzika kuliko kujiweka wewe pamoja na abiria wako katika hatari.

3. KUWA MWEPESI KUSOMA MAZINGIRA

Kwa lugha ya rahisi tunaweza kusema kuwa na machale. Yaani ni muhimu sana kuwa na uwezo wa kuchunguza mazingira uliyopo kwa haraka na kisha kutambua kama kuna hatari yoyote na kuchukua maamuzi ya haraka.

Kama upo peke yako katika eneo fulani hakikisha muda mwingi macho yako yanaangalia mazingira badala ya kuinamia simu tu muda wote.

Kama upo sehemu ambayo kuna kundi la watu kwenye giza wakiwa wanafanya shughuli ambayo haieleweki au ambayo unadhani kuwa ni ya hatari basi chukua maamuzi ya haraka ya kuhama.

4. EPUKA MITAA INAYOJULIKANA KWA UHALIFU

Kama umekuwa unaendesha abiria kwenye majukwaa ya usafiri kwa muda mrefu utakuwa tayari umesikia au unayafahamu yale maeneo ambayo yanajulikana kuwa na historia ya uhalifu.

Hata kama maeneo haya yana nauli kubwa jitahidi kutoelekea huko maana hauwezi kujua kitakachotokea. Epuka pia kupaki na kusubiri abiria usiku kwenye mitaa hatarishi ambayo haujawahi kufika au kusubiria abiria.

Kama kuna wahalifu wakiona gari geni ni rahisi kwao kuchukua hatua kwasababu wanajua hauwezi kuwafahamu.

5. EPUKA WATU WALIOLEWA SANA

Unapoenda kumfata abiria na ukakuta amelewa sana hadi hajitambui au anaongea kwa sauti sana, kwa fujo na hasa kama yupo peke yake au wote wamelewa hivyo hivyo ni bora kutowasafirisha.

Mambo mengi yanaweza kutokea abiria akiwa amelewa sana. Kwanza anaweza kukuletea fujo hadi kukuzuia kuendesha kwa umakini, anaweza kuanza kutapika sana. Pia anaweza kupata dharura ya kiafya na ukashindwa kumsaidia.

Anaweza akaleta shida kwenye kuelekeza anapoelekea na zaidi ya hapo unaweza kuishia kutakiwa kuzima gari na kumsaidia kushuka na kuingia nyumbani.

6. KUWA NA NAMBA YA POLISI

Mojawapo ya mbinu za usalama kwa madereva ni kuwa na namba ya polisi wakati wote. Kwa nchi nyingine hii wala sio tatizo lakini kwa nchi yetu watu wengi hata hawafahamu namba ya polisi ni ipi.

Hata kama namba ipo basi hadi polisi wafike eneo la tukio ni kazi kubwa sana. Kwa hiyo ikiwezekana chukua namba za polisi zaidi ya mmoja ili litakapotokea jambo ni rahisi kuwatafuta wakakupa msaada wa haraka.

7. NAMBA YA KAMPUNI YA USALAMA YA UBER

Kampuni ya Uber imeingia na ubia na kampuni ya usalama kutoa huduma ya security kwa madereva na abiria kwa masaa 24.

Bonyeza hapa kupata namba za simu na utunze kwenye simu yako

Hakikisha unawekuwa na namba hizi kwenye speed dial ili likitokea jambo lolote na ukahitaji msaada uweze kuupata ndani ya muda mfupi.

8. EPUKA MAKUNDI YA WATU

Unapoenda kuchukua abiria mmoja na ukafika ukute kundi la watu eneo hilo jaribu kuliepuka na kuegesha gari mbali nao.

Ukishaegesha gari mbali yao jaribu kuchuguza hali ya watu kwenye kundi hilo, kama kuna fujo, kupigana, kupandishiana ni bora ku-cancel safari kuliko kuchukua mtu.

Hii ni kwasababu kwenye hali kama hii ni rahisi kuingizwa kwenye ugomvi ambao haukuhusu. Pia ni rahisi kutokea kwa uharibifu wa gari lako kama kutakuwa na silaha kama chupa na mawe zinarushwa.

9. KUWA PROFESSIONAL

Kama ambavyo tumeshaongelea huko juu, wakati wa usiku watu wengi huwa wamelewa. Ni rahisi sana kwa wewe na abiria kupishana kauli kwasababu pombe huweza kufanya mtu akasirike haraka sana.

Kwa hiyo wewe kwasababu upo kazini unatakiwa kujitahidi sana kuwa mtulivu na kuongelesha abiria kwa ustaarabu wakati wote.

Jitahidi sana kutopandwa na hasira ingawa inaweza kuwa ngumu sana kuhudumia watu waliolewa bila kukereka.

10. GPS TRACKER

Ikitokea gari lako likaibiwa usiku ni ngumu kuweza kulipata tena kwasababu mara nyingi hakuna mashahidi wa kusema wameliona likielekea sehemu fulani.

Kifaa madhubuti katika kusaidia hili ni gps tracker. Hii itakusaidia kuona gari lako lilipo hivyo kusaidia polisi kulipata kiurahisi au kuwapata walioiba.

Ni muhimu kuzingatia mbinu za usalama kwasababu hauwezi kujua nini kinaweza kutokea unapokuwa unaendesha usiku.

Hatuwezi kushauri uache kabisa kuendesha abiria usiku kwasababu mara nyingi mida hii ndio maarufu kwa kuwa na safari nyingi zaidi na kwa bei nzuri. Ukiweza kuzingatia kila kipengele cha makala hii basi utakuwa unajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwa salama zaidi unapokuwa barabarani.

Je umewahi kupatwa na janga lolote wakati unaendesha abiria kwenye majukwaa yoyote ya usafiri wa ride sharing? Kama jibu lako ni ndio basi tafadhali tushirikishe ili na madereva wengine waweze kuchukua tahadhari.

Na kama makala hii imekusaidia kupata kitu kipya basi itakuwa vizuri sana kama uta-share post hii kwa madereva wengine kupitia whatsapp au mitandao ya jamii ili madereva wengine nao waweze kuja kujifunza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *