makosa wanayofanya madereva wanapokodi magari

MAKOSA 9 WANAYOFANYA MADEREVA WANAPOKODI MAGARI KWA WAMILIKI

Katika makala iliyopita tumechambua kiundani faida wanazopata madereva kwa kuanza biashara kwenye programu za safari kwa kutumia magari wasiyoyamiliki. Katika mwendelezo huu utaenda kuona makosa wanayoyafanya madereva wanapokodi magari kutoka kwa wamiliki.

Kwanza kabisa ni muhimu tukukumbushe kuwa sio madereva wote hufanya haya makosa yote unayoenda kuyaona. Wapo madereva wengi sana ambao ni wazoefu na hawapati shida yoyote katika kupata magari na wamiliki wazuri wa kuingia nao mikataba.

Makosa haya ndiyo ambayo uchunguzi wetu umeona kuwa yanafanywa na wengi zaidi. Na lengo kuu la makala hii ni kusaidia madereva wapya waweze kujiepusha nayo ili wajiweke katika nafasi nzuri zaidi ya kufurahia ushirikiano wao na wamiliki wa magari wanayoendesha.

MAKOSA WANAYOFANYA MADEREVA WAKATI WA MAKUBALIANO NA WAMILIKI MAGARI

1. Kutomchunguza mmiliki wa gari

Kabla ya kuingia mkataba na mtu yeyote yule ni muhimu sana kumfahamu angalau kwa undani kidogo. Madereva wengi huwa na haraka ya kupata gari na kuanza biashara kiasi kwamba hupokea ofa ya kazi kutoka kwa mtu yeyote yule. Hii ni hatari sana kwa sababu katika maisha chochote kinaweza kutokea.

Hata mwenye gari pia hawezi tu kukodisha gari lake kwa dereva yeyote yule bila kumchunguza. Hata hayo majukwaa ya programu za safari huchunguza madereva ingawa sio sana kabla ya kukubali maombi yao ya usajili ila lazima wajihakikishie wamepata taarifa za kujitosheleza.

Vitu vichache tu vya kufahamu kuhusu mtu anayekukodisha gari ni kama vifuatavyo:

  • Majina yake kamili
  • Umiliki wake wa gari: Je gari ni lake kweli au la mtu mwingine?
  • Kazi yake au shughuli anazofanya
  • Mahala anapoishi
  • Mahala pa kazi au biashara
  • Namba za simu, anwani ya barua pepe au sanduku la posta.

Hivi ni baadhi tu ya vitu ambavyo angalau unatakiwa kuvifahamu kabla ya kuingia makubaliano ya kukodi gari kutoka kwa mtu yoyote.

2. KUTOCHUNGUZA GARI

Kabla ya kukubali kukabidhiwa gari ni muhimu sana kwa dereva kulichunguza kiuzoefu na kiufundi. Kama hauna uzoefu sana na magari basi ni bora utafute fundi mtaalamu akakusaidie kulikagua mbele ya mwenye gari.

Madereva wanapokodi magari wanapaswa kuhakiki vitu vituatavyo muhimu kwenye gari:

  • Nyaraka zote za gari: je zimetimia? Je majina kwenye nyaraka yanaendana na majina ya mmiliki unayeingia naye mkataba au la?. Kama majina hayaendani basi mmiliki sahihi ameridhia gari au chombo chake kikodishwe? Je nyaraka kama bima zipo up-to-date au zinaisha ndani ya muda mfupi? Unakuta mtu anakodisha gari huku bima imebaki wiki moja tu iishe. Hii italeta usumbufu, ni bora nyaraka zote ziwe up-to-date wakati wa kuweka saini kwenye mikataba.
  • Vifaa vya kwenye gari: Kagua redio, siti, mazulia hadi vifaa muhimu kama triangle, fire extinguisher, vifaa vya matengenezo kama jeki, tairi la ziada, spana nk. Unatakiwa kutambua vifaa vilivyopo, vinavyokosekana pamoja na ubora wa kila kimoja.
  • Ubora wa gari: Kagua gari kuanzia nje hadi ndani, kila kitu kipo sawa? kuna mikwaruzo au ubovu?

Madereva wengi sana aidha hawakagui au huwa wanakagua juu juu tu kwa haraka ya kuanza biashara. Hii ni hatari sana kwa sababu unajiweka kwenye nafasi nzuri kabisa ya kubebeshwa lawama pale hitilafu zitakapotokea au itakaposemekana umerudisha gari na ubovu hata kama inaweza kuwa si kweli.

3. Kutojaribu kuendesha gari kwanza

Baada ya kuona gari ni muhimu sana kumuomba mmiliki uingie naye na mfanye safari fupi pamoja ili kuona hali ya gari kabla ya kukodi gari. Na majaribio haya yanatakiwa kufanywa kwenye barabara nzuri na mbovu pia maana kuna magari ambayo yanakuwa vizuri tu kwenye barabara za lami lakini kwenye mashimo hayafai kabisa.

Wakati wa kuendesha unatakiwa kusikilizia ugumu au wepesi wa gari, harufu na sauti linalotoa. Kama vile haufahamu sana kuhusu magari basi kama tulivyosema hapo awali, nenda na fundi unayemwamini akusaidie kuchunguza.

Madereva wengi sana wameishia kusaini mkataba na magari mabovu ambayo wanaishia kushinda nayo gereji tu.

4. Kutochagua aina ya gari

Madereva wanapokodi magari mara nyingi huwa wamekuwa wakitafuta gari muda mrefu tayari. Hii husababisha dereva kukubali gari lolote lile ambalo mmiliki atajitokeza nalo kutafuta dereva.

Ubaya wa hili ni kwamba sio kila magari yana faida nzuri kwa kufanya biashara ya kuendesha abiria kwenye majukwaa ya programu za safari.

Kwa mfano, yapo magari ambayo hutumia mafuta mengi zaidi hivyo kupunguza faida kwa kutumia pesa nyingi kuendeshea biashara. Yapo pia magari madogo sana ambayo abiria wengi hulalamika nafasi ndogo au kubanwa miguu.

Hakikisha unafahamu magari ambayo hayana gharama kubwa zaidi za uendeshwaji na matengenezo ili kuhakikisha haupati hasara wakati wa kuamua kiasi cha kugawana na mwenye gari.

5. Kutofanya makubaliano sahihi

Suala la kukodisha gari si suala dogo. Madereva wengi huingia kwenye makubaliano na wamiliki wa magari kwa njia ya kujuana tu badala ya kuandaa mikataba sahihi inayotambulika kisheria.

Ndio unaweza kuwa na mikataba ya maneno lakini lazima uwepo ushahidi wa makubaliano haya kwa maandishi au rekodi ya video au sauti. Magari na vyombo vya moto kwa ujumla yana gharama kubwa sana. Kutokana na hili ni lazima kuwepo na mkataba la sivyo kuna uwezekano wa mtu kuja kuangukiwa na jukumu kubwa sana kupokea hasara.

Kama mmiliki wa gari anaweza kulipa mwanasheria kuandaa mkataba basi dereva unapaswa kuupitia mkataba ule kwa utulivu kabisa ili kuhakikisha unakubaliana na kila kipengele.

Kama hauwezi kuchambua vizuri mikataba ni bora kutafuta mtu ambaye ana ujuzi huu ili kukusaidia usiwe wewe kwenye upande wa kugharamia hasara pale tatizo litakapotokea.

6. Kutofanya uchunguzi wa mgawanyo wa faida

Baadhi ya madereva wanapokodi magari kwa wamiliki huwa wanasahau sana kufanya uchunguzi wa njia sahihi na kima sahihi cha kuwalipa wenye magari.

Kabla hata ya kuanza kutafuta gari dereva unapaswa kufahamu madereva wengine wanaotumia magari ya kukodi huwa wanagawana kiasi gani na wenye magari.

Pia wakati wa kukubaliana kiwango hiki ni muhimu kukumbuka kuzingatia uzoefu wako wa kuendesha abiria kwenye majukwaa ya programu za usafiri.

Madereva wenye uzoefu mkubwa zaidi wanategemewa kupata hela nyingi zaidi kuliko wale wageni kwasababu

  • Wanajua mbinu za kupata biashara zaidi.
  • Wanajua njia nzuri na maeneo yenye abiria wengi zaidi
  • Ni salama zaidi kwa wamiliki kuwapa magari yao kwa sababu tayari wanajua kuwa wana historia ndefu na wamiliki wengine.

Kwa hiyo kama wewe ni mzoefu jaribu kuuliza madereva wenye uzoefu kama wewe huwa wanagawana kiasi gani na wamiliki wanapoingia mikataba nao.

Pia unapoulizia watu kiasi wanachogawana na wamiliki usisahau kuulizia na aina za magari wanayotumia. Kama ambavyo tumeshasema mara nyingi sana katika makala zetu nyingine magari tofauti yana gharama tofauti za uendeshaji. Kwa hiyo hata kiasi cha mgawanyo inabidi kitofautiane kama magari ni tofauti.

7. Kutopigania maslahi

Madereva wengi hukubaliana tu na kiasi wanachopanga wamiliki bila kujitetea kama kiasi hicho hakina uhalisia kwao. Hata kama ndio unahitaji gari uanze biashara haimaanishi kuwa unatakiwa kukubali tu kutumika na kupata hasara pamoja na msongo wa mawazo.

Kama mmiliki hajazingatia mambo muhimu katika kuamua kiasi anachotaka kuletewa kwa wiki au siku basi ni jukumu lako kumuelekeza na kumuonesha njia sahihi za kusesabu malipo pamoja na mifano hai.

8. Kutokuwa na mashahidi

Kabla ya kukabidhiwa gari ni muhimu sana kuhakikisha upo ushahidi wa kutosha juu ya hali ya gari wakati wa kukabidhiwa. Madereva wengi sana katika na haraka ya kupata gari huwa wanaruka hatua hii ya muhimu sana.

Ushahidi unaweza ukawa wa mtu kuwepo kwa ajili ya kila upande mfano mjumbe wa nyumba kumi au mwanasheria. Pia ushahidi unaweza kuwa kwa njia ya picha au video zenye muhuri wa tarehe.

Hii husaidia sana kuepusha matatizo wakati wa kurudisha gari.

9. Kutojenga mahusiano mazuri na wamiliki

Moja ya viashiria vya ushirikiano mzuri kati ya wamiliki na madereva ni kuwa na mahusiano mazuri hasa kwa kuzingatia mawasiliano ya mara kwa mara. Makubaliano yanatakiwa kuwekwa kuanzia mwanzo kuhusu njia za mawasiliano na muda sahihi.

Tangu mwanzo ni muhimu sana kuzingatia matakwa anayoweka mwenye gari kwasababu gari limeingia gharama kubwa sana kwake.

Kama mtaamua kuwa mmiliki anataka mahesabu kila siku au kila wiki au kila mwezi hakikisha upo tayari kuafiki na kutimiza. Kama atataka gari lake liegeshwe nyumbani kwake na sio uendeshe usiku kucha pia hakikisha upo tayari kwa hilo.

Kama kuna lolote hauliafiki ni bora kutokubali au kuomba mabadiliko kuliko kuja kukwazana naye hapo mbeleni.

10. Kuto Update mikataba

Madereva wanapokodi magari kwa wamiliki mara nyingi huwa na mkataba ambao hujumuisha vipengele vyote vya ushirikiano huu. Mara nyingi sana mabadiliko hutokea huku duniani ambayo huwa yanasahaulika kuingizwa kwenye mkataba au yanaingizwa kwa maneno tu ya juu juu bila kubadili mkataba wa mwanzo.

Mfano mkubwa ni bei ya mafuta kuongezeka.

Kila bei inapoongezeka inabidi itajwe kwenye mkataba kwa sababu mara nyingi mafuta hupanda bei bila nauli kuongezeka. Hii husababisha dereva kupata hasara kwa sababu katika mkataba anatakiwa kukabidhi kiasi fulani kwa mwenye gari bila kujali yeye atabaki na kiasi gani.

Mfano mwingine ni Kupanda kwa tozo za kutuma na kutoa hela kidijitali.

Unaweza kusema mabadiliko ni madogo lakini ukikaa ukapiga mahesabu kwa siku, kwa mwezi na kwa mwaka ni kiasi gani kinakatwa kwenye miamala wakati wa kutoa au kutuma hela kwa mwenye gari utapigwa na butwaa.

Pale mabadiliko yoyote yatatokea lazma makubaliano yabadilishwe na rasmi na mashahidi wawepo.

Ni muhimu sana kutia maanani makosa haya pale madereva wanapokodi magari kwa mtu yeyote yule hata kama unafahamiana naye. Mwanzo wakati wa kukabidhiana gari mnaweza kuwa na mahusiano mazuri lakini hauwezi kujua huko mbele kinaweza kutokea kitu ambacho kinaweza kuingilia kati na kusababisha matatizo.

Je, umewahi kukodi gari kwa ajili ya kufanya biashara katika programu za safari? Ulifanya makosa yoyote kati ya haya tuliyojadili?

Tafadhali tushirikishe ili na sisi pamoja na madereva wengine tujifunze kutokana na uzoefu wako.

2 thoughts on “MAKOSA 9 WANAYOFANYA MADEREVA WANAPOKODI MAGARI KWA WAMILIKI”

  1. Kwenye wallet yangu Kuna ujumbe huu ujumbe mbona siuelewe naomba ufafanuzi (payment to Uber) alafu ndani ya masaa 72

    1. Habari Bwana Hafidh?

      Pole kwa changamoto uliyoipata. Kwa upande wetu tunakushauri uwasiliane na kampuni husika iliyokutumia ujumbe wako kwa kutumia njia ya mtandao au kwa kutembelea ofisi zao, ili uweze kupata maelezo yaliyokamilika. Asante

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *