madereva uber wengi wanaapata changamoto

MADEREVA UBER WENGI WANAACHA KAZI KWA SABABU HIZI.


Ukilinganisha na nchi za nje, madereva wengi wa Uber hapa Tanzania huvumulia mengi sana na kuendelea na kazi hata pale matatizo yanapozidi.

Ripoti zinaonesha kuwa mwaka 2020 tu kuanzia Januari hadi Aprili Uber ilipoteza 60% ya madereva wake. Hii inawezekana kuwa ilichangiwa na mlipuko wa gonjwa la UVIKO 19 lakini hata kabla ya hapo, tafiti zinaonesha kuwa 50% hadi 70% ya madereva Uber wamekuwa wakiacha kazi kila mwaka kuanzia kuanzishwa kampuni hiyo.

KWANINI MADEREVA UBER WENGI WANAACHA KUENDESHA?

Jibu la swali hili ni tofauti kulingana na sehemu waliopo madereva hawa. Kwa mfano katika nchi zilizoendelea, sababu kuu za madereva kuacha kazi ni kama zifuatazo:

1. UDEREVA WA MUDA (PART TIME)

Soko la ajira katika nchi za nje ni tofauti sana na Tanzania. Kule mtu anaweza kuamua kufanya ajira kwa masaa fulani na masaa yanayobaki kufanya ajira nyingine au shughuli nyingie kama kusoma.

Madereva Uber wengi kwenye nchi hizo hawafanyi kazi hii full time, wengi ni wanafunzi, waajiriwa au tayari wana shughuli nyingine ambayo inawaingizia kipato.

Kutokana na hii, asilimia kubwa ya madereva wa huko huacha kuendesha Uber kutokana na kwamba wanapata kazi nyingine zenye malipo makubwa zaidi.

2. KERO ZA ABIRIA

Watu wengi wa nchi za nje wamezoea ustaarabu katika utoaji wa huduma. Lakini wewe kama dereva utakuwa tayari unafahamu kuwa mara nyingi sana abiria huwa si wastaarabu kabisa. Wengi wao wanajua kuwa kampuni inachukulia mteja kama mfalme ambaye hakosei hivyo kupelekea kuwakosea heshima madereva.

Hii husababisha madereva wengi kuacha shughuli hii kwasababu na wao wameshazoea kupewa huduma kistaarabu huko nchini kwao.

3. KERO ZA KAMPUNI

Madereva wa nchi za nje wanajua kuwa zipo sheria zinazowalinda na uonevu wa waajiri au makampuni. Kwa hiyo pale ambapo wanaona kampuni inawaonea kwa lolote lile huwa hawawezi kuvumilia.

Tofauti na nchini kwetu ambapo madereva wanahitaji zaidi fursa hii, hivyo wengi hulazimika kuvumilia zaidi hata pale ambapo wanaonewa.

SABABU ZA MADEREVA UBER WENGI TANZANIA KUKATA TAMAA NA KUACHA KAZI

1. ALGORITHM

Algorithm ni seti ya misingi au sheria zinazotakiwa kufatwa katika kupiga mahesabu, kutatua tatizo au kufanikisha shughuli fulani hasa katika vifaa vya teknolojia.

Mfano wa jinsi algorithm ya Uber inavyofanya kazi ni katika kuchagua madereva wapi wapewe safari nyingi zaidi.

Ili kupata safari nyingi zaidi zipo sheria kama kuwa na alama nzuri ya nyota, kuwa na comment nzuri za abiria waliofurahia huduma, kuwa umeendesha Uber kwa muda mrefu, kutokuwa na malalamiko nk

Hizi zote ni sheria au misingi ambayo teknolojia ya application ya Uber inatumia kukagua na kuchagua madereva bora kwa ajili ya abiria wao ili wafurahie huduma.

Madereva wengi sana hasa wapya hupata changamoto kidogo kuelewa kuhusu algorithm ya Uber ilivyo na jinsi ya kuitumia kufanikiwa zaidi kwa kupata safari nyingi zaidi.

Kutokufahamu hupelekea kukata tamaa hasa pale yanapotokea mabadiliko kama nauli kushuka na kutopata abiria. Madereva wengi wa nchi za nje hujifunza sana kuhusu algorithm na Uber na jinsi ya kupata mafanikio kupitia ufahamu huu.

Ndio maana hata ukienda google au youtube utakuta blog nyingi sana na channel nyingi sana zinazoelekeza kila kitu juu ya kipengele hiki kwa ufanisi na undani sana. Na pia kwenye comments utakuta madereva wengi sana wakijifunza na kubadilishana mawazo kuhusu mbinu hizi.

Sisi hapa Weibak tumejikita katika kusambaza taarifa na mafunzo yanayoenda na wakati na jinsi ya kupata mafanikio makubwa kwenye majukwaa haya ya usafiri.

Kwa hiyo usijali kabisa, hakikisha tu unajisajili ili kupata email za makala mpya za mafunzo ambayo yatakusaidia sana katika kuli master jukwaa lako lolote la ride hailing!.

2. JIOGRAFIA

Kusema ukweli hizi huduma za usafiri zinazotumia sana teknolojia zimeundwa kwa ajili nchi za nje na zinafaa zaidi kwenye nchi hizo ambapo miji yote hadi mitaa inafahamika na kufikika kirahisi.

Nchi za nje dereva Uber anaweza kufika hadi mlangoni kwa abiria kumfata au kumrudisha bila hata kuwa mwenyeji au mzoefu wa eneo kwasababu kila eneo lina jina na namba maalumu, na pia linaonekana kirahisi kwa kutumia ramani na gps.

Nchi kama Tanzania bado sana kufikia viwango hivi. Zipo changamoto hata katika kumfikisha abiria kwenye maeneo husika kama dereva si mzoefu sana.

3. MIUNDOMBINU

Tunaendelea na suala lile lile la kwamba Uber na makampuni mengine ya ride hailing kuwa yameundwa kufanikiwa nchi za nje. Madereva wa Uber Tanzania wana changamoto na hasara kwasababu miundo mbinu kama bara bara ina athiri sana faida ya kuendesha abiria.

Nje ya nchi ni rahisi sana kuhesabu dereva anatengeneza kiasi gani kwa lisaa limoja. App ikisema safari ni ya lisaa moja inakuwa kweli ya lisaa moja kwasababu bara bara zao ni nzuri na hazina foleni sana, hivyo kuleta ufanisi na urahisi wa kukisia muda wa safari.

Nchini kwetu safari ya lisaa limoja inaweza kugeuka kuwa safari ya masaa matatu kwasababu ya ubora bara bara na hali ya barabarani. Foleni, magari kuharibika na kuziba njia, kusimamishwa na polisi wa barabarani, kufurika kwa maji wakati wa mvua kali, ubovu wa barabara na mengine mengi huleta changamoto kubwa sana kwa madereva.

Hii hupelekea madereva wengi kukata tamaa kwasababu mwisho wa siku dereva anakuwa barabarani kwa masaa mengi huku akiingiza pesa ambayo haiendani kabisa na muda aliotumia.

4. ADHABU

Kama ambavyo tumechambua mara nyingi sana katika makala zetu, kampuni yoyote ile duniani huheshimu na kuwapa kipaumbele wateja huku watoa huduma wakiwekwa nyuma.

Moja ya kero kubwa sana inayosababisha madereva Uber wengi kuacha kazi ni adhabu kali ambazo Uber hutoa kwa madereva. Endapo abiria atalalamika, hata kabla ya uchunguzi kuanza tayari akaunti ya dereva huwa inasimamishwa.

Mara nyingi madereva hawastahili adhabu hizi kabisa! na wengi wanalalamika sana juu ya hili. Wakati mwingine kunaweza kuwa na hitilafu katika application ambazo hupelekea akaunti za madereva kufungwa bila hata sababu za msingi.

Juu ya haya yote, hatua za kuondoa adhabu na kurudisha akaunti nayo ni ndefu sana, hivyo kupelekea madereva ambao wanakuwa wameadhibiwa kimakosa kuamua kuacha tu.

5. MAWASILIANO

Ukilinganisha na kampuni nyingine za usafiri wa ride hailing Tanzania, katika kampuni ya Uber ni ngumu zaidi kupata mawasiliano na uongozi.

Hii ni kwasababu kwanza ofisi zao zipo kwenye jiji moja tu la Dar es salaam, pili kurasa zao za mitandao ya jamii ni kama tu hazina huduma au hazipo kabisa.

Hii inaleta changamoto kubwa sana kwa madereva kwasababu wengi huwa wanahitaji masuluhisho ya haraka hasa kwenye suala zima la kufungiwa akaunti au hitilafu za mahesabu ya nauli.

Pia changamoto hii hupelekea madereva kuona kwamba hawasikilizwi kwasababu ni kama hakuna njia ya kuwasilisha malalamiko na kusikilizwa.

Mara nyingi madereva wamefikia mahala ambapo wameamua kugoma kufanya kazi ili tu kuhakikisha wanaweza kusikilizwa na matatizo yao kutatuliwa.

Kwa kifupi tu haya ndio makundi makuu ya sababu za madereva Uber wengi kuacha kuendesha abiria kwenye jukwaa la Uber Tanzania.

SOMA HAPA KWA UNDANI: Changamoto za madereva Uber Tanzania 2022

Je, umewahi kutamani kuacha kuendesha abiria wa Uber na kuhamia kampuni nyingine? Kama ndio, ni nini kilikusababisha kuona ni bora tu kuacha?

2 thoughts on “MADEREVA UBER WENGI WANAACHA KAZI KWA SABABU HIZI.”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *