Kampuni ya Bolt Tanzania kwa kupitia mpango wake wa green plan inahamasisha madereva Bolt watumie gesi badala ya petroli ili kusaidia mazingira na kuinua uchumi.
Meneja wa Bolt nchini, Remmy Eseka alisema jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa “Kupitia Mpango wa Kijani wa Bolt, kitendo cha madereva kwenye jukwaa letu kuanza kuchukua hatua ya kutumia CNG ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kupigania kutengeneza miji bora huku tukiwajengea uwezo madereva wetu na kuwapatia fursa bora za mapato”.
FAIDA ZA KUTUMIA GESI ASILIA BADALA YA PETROLI
GHARAMA: Bei ya gesi asilia ni nafuu sana ukilinganisha na bei ya petroli. Hadi leo bei ya gesi inakaribia nusu ya bei ya petroli . Kwa hiyo kwa kutumia gari lenye injini inayoendeshwa na gesi, dereva Bolt anaweza kutengeneza faida kubwa sana kwasababu ya kupunguza gharama ya uendeshaji.
Zaidi ya hayo, Lita moja ya petroli ambayo ni tsh (2,501/= – 2,750/=) inaweza kusafirisha gari umbali wa kilomita 12 wakati kiasi hicho hicho cha gesi asilia ambacho kina bei ndogo zaidi (1,500/=) kinaweza kuendesha gari umbali wa zaidi ya Kilomita 20.
GHARAMA YA MATENGENEZO
Zaidi ya yote kwasababu gesi asilia ni safi, inapunguza sana uhitaji wa matengenezo ya gari ya mara kwa mara. Magari yanayotumia gesi yanatakiwa kufanyiwa matengenezo au ukarabati wa kawaida kila baada ya kilomita 6,000.
SOMA: BEI MPYA ZA PETROLI, DIESEL NA MAFUTA YA TAA KWA KILA MKOA KUANZIA JAN 2022 KUTOKA EWURA.
UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Gesi asilia ni safi na inapowaka haileti masizi au kaboni kama petroli inavyotoa moshi. Kaboni huharibu mazingira kwa kudhuru tabaka la Ozoni ambalo ndilo linakinga mionzi ya jua hatarishi kutufikia.
Kwa hiyo ni vizuri madereva Bolt watumie gesi badala ya petroli kwa ajili ya faida yao na nchi pia.
Pia kwasababu magari yanayotumia gesi hayatoi moshi mzito uliojaa kaboni, hewa safi ya oksijeni inakuwa nyingi zaidi hivyo kupelekea hali nzuri ya upumuaji kwa watu wote.
Meneja wa Bolt Tanzania amesema kuwa karibuni kutakuwa na kitengo cha wapanda Bolt za kijani yaani zisizotumia petroli/diesel, pia bajaji za umeme na baiskeli za kielektroniki. Yote haya ni kwa ajili ya kusaidia kuokoa mazingira, kupunguza gharama za nauli na kuongeza faida kwa madereva.
HII INA MAANISHA NINI KWA MADEREVA?
Kampuni yoyote inapoonesha muelekeo kama huu huwa kuna faida sana kwa wadau wanaoitikia mwito.
Hii ni kwasababu kampuni itaanza kuwapa kipaumbele zaidi madereva ambao watakuwa wanatumia gesi asilia kwa kuwapa safari nyingi zaidi. Pia kwasababu nauli zitakuwa tofauti kiasi kwamba abiria nao watakuwa wanapendelea zaidi bolt green kuliko za kawaida.
Kwa hiyo hii ni kama kampeni ambayo itaendelea mpaka pale kutakapokuwa na magari mengi zaidi kwenye jukwaa la Bolt yanayotumia gesi.
GESI ASILI NI SALAMA KUENDESHEA GARI?
CNG (Compressed Natural Gas) sio kama hii gesi tunayotumia kupikia majumbani. Hii ni gesi salama na imekuwa ikifanyiwa utafiti kwa miaka 11 kabla ya kuanza kutumika hapa Tanzania.
Gesi hii ni nyepesi zaidi, mtungi wake ni mgumu sana hata risasi haiwezi kuutoboa na huu hufungwa na wataalamu nyuma ya gari sehemu ya mizigo.
Utafiti pamoja na ufungaji mitungi ya gesi kwenye magari ulikuwa ukifanyika katika kitengo maalumu cha gesi asilia katika taasisi ya teknolojia Dar es salaam (DIT).
Mpaka sasa wataalamu wenye kibali cha kufunga huduma hii kwenye vyombo vya moto wana viwango vya kimataifa na wapo watatu tu Tanzania nzima.
Pia usalama wake ni wa hali ya juu, hata dereva hawezi kujaziwa gesi kama hana stika maalumu ya kibali cha uthibiti mfumo wa gesi kutoka kwa mmoja kati ya hawa wataalamu wa gesi asili.
Magari size zote yanaweza kufungiwa mtungi na kuanza kujivunia faida ya nishati hii nafuu.
GHARAMA ZA KUWEKEWA MTUNGI
Mratibu wa kitengo cha gesi asilia DIT Dr. Esebi Nyari amefafanua kuwa gharama za kuweka mfumo wa nishati ya gesi asilia ni tofauti kutokana na ukubwa wa gari.
Katika mahojiano na waandishi wa habari amesema kuwa magari madogo yenye silinda nne, mengi hulipia kuanzia 1,800,000/= tsh huku magari makubwa yenye kuanzia silinda 6 gharama yake ya kubadili mfumo wa nishati huanzia 2,000,000/= tsh na magari yenye silinda 8 hutozwa tsh 2,400,000/= kwa huduma.
Unapofunga mfumo wa nishati ya gesi hamaanishi kwamba hauwezi tena kutumia mafuta pale unapahitaji.
Mfumo wa mafuta bado unakuwa pale pale na muda wowote unaotaka kubadilisha nishati unabadilisha tu bila shida.
Gharama hii ni nafuu sana na ndani ya miezi mitatu tu utajikuta hela yako yote imerudi kwasababu utaweza kuokoa gharama ya mafuta kwa kiasi kikubwa sana!
Ufundi pia hauchukui muda mrefu. Ndani ya siku mbili gari linakuwa tayari kwa kuendelea na biashara na kukusanya faida kubwa zaidi.
MADEREVA WA MAJUKWAA MENGINE WANATUMIA GESI ASILI?
Moja ya makampuni ya kwanza kusapoti kazi ya taasisi ya DIT juu ya ufungaji mfumo wa gesi asili kwenye magari ni Uber. Madereva wengi wa Uber wamekuwa wakitumia gesi badala ya mafuta na wamesema kuwa wamekuwa wakitengeneza faida kubwa sana!
Mmoja wa madereva wanaotumia jukwaa la Bolt kwa miaka miwili sasa, Amri Mkiwa alisema, “Tangu nianze kutumia CNG, mapato yangu hasa wakati wa kutumia Bolt App yameongezeka kwa 85% kwani gharama zangu zimepungua sana. Kwa sasa natumia 15,000/= kujaza gesi, lakini hapo awali ningetumia 30,000/= hadi 35,000/= kujaza petroli. Ningependekeza sana madereva wengine kubadili na kutumia CNG,“
Elias Mruma, dereva mwingine wa Bolt alisema “Kupitia matumizi ya CNG, nimeweza kupunguza gharama, kuongeza mapato yangu na kuwapeleka watoto wangu wawili shule za kimataifa,
Juu kabisa, naweza kutumia hadi 17,500/= kujaza gari na gesi, na kuniwezesha kupata angalau 70,000/= kwa siku nikitumia jukwaa la Bolt.
Kwa hiyo, matumizi ya gesi asilia yanasaidia kupunguza gharama za mtu kwa “asilimia 75”
Kweli kabisa kuna faida kubwa sana kibinafsi na kwa mazingira katika kubadili kutoka kutumia mafuta kwenda kutumia gesi asilia kwenye magari.
Hapo mwanzo kampuni ya Uber kushirikiana na benki mojawapo kubwa Tanzania ilikuwa inatoa huduma ya kubadilishiwa mfumo kwa madereva wake kwa mkopo wa kulipwa kidogo kidogo.
Inawezekana sana kuwa hapo mbeleni kampuni ya Bolt pia itafanya mchakato wa kusaidia madereva watumie gesi badala ya petroli kwa kutoa msaada wa kifedha kama Uber.
Endelea kutembelea Weibak Carsharing na kujisajili ili upate email kila makala mpya za uchambuzi na elimu ya biashara ya ride hailing zinapochapishwa.
Kwenye sehemu ya comments tushirikishe kama wewe unatumia gesi asilia kwenye gari lako, au kama unafahamu dereva yeyote anayetumia.
Kama vile una maswali yoyote au kama ungependa kufahamu zaidi kuhusu Bolt green plan wasiliana na uongozi kwa kupitia njia HIZI.
Pia tushirikishe kama ungependa kufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kupata mkopo wa kuweka mfumo wa gesi kwenye gari lako ili utengeneze faida kubwa zaidi.
Pingback: BOLT IMEONGEZEWA UFADHILI WA TRILIONI 1.5 - Weibak Carsharing
Mm nilikua anaendesha Gali kutokana na changamoto kwa Sasa nipo na boda boda na kazi zinafanyika Kama kawaida milikuwa na uliza up mfumo wa gesi uwezi tumia kwenye pikipiki Mana mfuta changamoto kidogo