Dereva Uber/ Bolt akijaza fomu

KILA DEREVA WA UBER/BOLT ANAPASWA KUJIULIZA MASWALI HAYA

Kila siku madereva wapya wanajisajili kuanza kuendesha abiria kwenye majukwaa ya Ride sharing. Ili kuwa wakipekee inabidi kila dereva wa Uber/Bolt ajiulize maswali sahihi na awe na majibu yake kabla hajaanza au hajaendelea na kazi hii.

Kupata mafanikio na kutengeneza pesa nyingi kwa kuendesha Uber si kitu rahisi sana. Inahitaji bidii ya ziada na ufahamu wa vitu ambavyo vitakufanya uwe wa aina yake katika sekta hii yenye ushindani mkubwa.

Hapa Weibak Carsharing tumebobea katika kukusanya na kuchambua habari zote kuhusu sekta hii ya usafiri wa kushirikiana. Lengo letu kubwa ni kusaidia madereva na wamiliki magari kupata elimu sahihi na taarifa zote za jinsi ya kupata mafanikio makubwa katika majukwaa ya usafiri kama Uber/Bolt nk.

Katika makala hii tumekuandalia maswali yote muhimu ambayo madereva wengine wa Uber wamekuwa wakiuliza. Haya yatakusaidia na wewe kutatua changamoto kabla hata haujazifikia na pia yatakuweka kwenye nafasi ya kutengeneza pesa zaidi.

KILA DEREVA WA UBER/BOLT ANATAKIWA KUJIULIZA MASWALI YAFUATAYO:

1. NINAWEZAJE KUPUNGUZA GHARAMA ZA UENDESHAJI?

Ili kupata faida kubwa zaidi kwa kuendesha gari Uber/Bolt ni lazima kujua unatumia kiasi gani kwa ujumla katika kutoa huduma.

Usipokuwa makini unaweza kukuta unatengeneza faida ndogo au hata unapata hasara kutokana na kutumia gharama kubwa sana kusafirisha abiria.

Gharama za kuendesha Uber/Bolt zinagawanyika katika sehemu zifuatazo:

  • 1. Gharama za Dereva: Vitu vyote unavyonunua wakati wa kazi kwa mfano chakula na vinywaji.
  • 2. Gharama za abiria: Vitu vya kuvutia wateja kama huduma na vifaa vya kuchaji simu, maji ya kunywa nk
  • 3. Gharama za gari: Mfano kununua mafuta, kusafishiwa gari (Car wash) na huduma za ziada kama kujaza upepo kwenye matairi.

Hizi zote ni gharama za muhimu sana ambazo ukizizingatia na kuweka mkakati wa kuzipunguza unaweza kutengeneza faida kubwa zaidi.

Jinsi ya kupunguza gharama za dereva:

  • Tafuta sehemu wanayouza chakula kwa bei nzuri: kama kila siku unanunua chakula basi ndani ya mwezi au mwaka utakuwa unatumia hela nyingi sana ambayo ingeweza kuwa faida ya kuendesha abiria.
  • Beba chakula kutoka nyumbani: Au rudi nyumbani muda wa chakula ule kisha uendelee na kazi. Unaweza kubeba snacks ndogo ndogo pamoja na maji ya kunywa pia ili kuepusha kununua mara kwa mara.

Jinsi ya kupunguza gharama za gari:

  • Vituo sahihi vya mafuta: Chunguza bei ya mafuta kwenye sheli zilizo karibu nawe. Unaweza kuona tofauti ni ndogo sana lakini ukipiga mahesabu ni mara ngapi kwa mwezi au hata kwa mwaka unaweka mafuta, utagundua kuwa unaokoa hela nyingi sana.
  • Fanya service ya gari: Gari lako likiwa linafanyiwa service nzuri kwa muda sahihi basi litakuwa haliharibiki hovyo hivyo kupunguza gharama ya kuliendesha.
  • Garage moja nzuri: Ukiwa mteja wa kurudia rudia wa garage moja ni rahisi kupata huduma nzuri kwa punguzo la bei. Mfano mzuri ni huduma ya kuoshewa gari nje na ndani. Mara nyingi watoaji huduma hii hupenda wateja wao warudi mara kwa mara hivyo hutoa punguzo kwao.

2. NIFANYE NINI ILI GARI LANGU LIWE SAFI MUDA WOTE?

Abiria wote hupenda magari masafi na yenye harufu nzuri. Kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha unawafurahisha na wanakupatia ratings/alama za juu kwenye profile yako ya Uber au Bolt

Kama tulivyosema hapo juu, kuwa mteja wa kurudia wa sehemu moja nzuri inayotoa huduma ya kusafisha gari. Hii itapunguza gharama na kuhakikisha gari lako ni safi na linanukia vizuri muda wote.

Pia ni muhimu kuwa na vifaa vidogo vidogo vya kufanya usafi wa haraka pale unapokuwa unasubiria abiria wapya. SOMA HAPA aina za vifaa muhimu ambazo kila dereva wa Uber/ Bolt anatakiwa kuwa navyo kwenye gari.

3. NINATAKIWA KUMUHUDUMIA VIPI ABIRIA WA UBER/BOLT?

Kila dereva wa Uber/Bolt anapaswa kufahamu vitu sahihi vya kufanya na kuepuka kwa abiria wake. Ni muhimu sana kuwa mstaarabu, kusalimia na kuwakaribisha wateja wako.

Usilazimishe au usiombe tip/motisha, badala yake jitahidi kumpatia huduma bora hadi yeye mwenyewe apendezwe na aguswe kukupatia motisha.

Njia nyingine ya kupata motisha na ratings nzuri ni kumpa mteja vitu vidogo vya bure kama huduma ya kucharge simu, vitu vidogo vya kutafuna kaka pipi na bubblegum au hata maji ya kunywa.

PITIA: Sheria za utoaji huduma Uber/Bolt

4. NIWAPE ABIRIA ALAMA GANI?

Madereva wa Uber pamoja na abiria wanaweza kupeana alama au ratings kutokana na wanavyoona inafaa.

Ni muhimu wote madereva na abiria kupewa alama nzuri kwasababu alama mbaya zinapunguza uwezo wa kupata abiria wengi kwa dereva, na kwa abiria inapunguza uwezo wa kupata magari ya kupanda kwasababu hakuna mtu anapenda shida na wenzake.

Ingawa abiria wengi wanaweza kuwa si wastaarabu na wakawa wanakukosea mara kwa mara, inashauriwa usiwe unawapa maksi mbaya sana mara kwa mara.

Badala yake ni bora usimpe mtu alama kabisa kuliko kutoa alama mbaya mara nyingi. Hii ni kwasababu wakati mwingine abiria anakuwa tu na matatizo mengi kichwani kwa hiyo kwa bahati mbaya anashindwa kujizuia wakati anakutana na watu wengine.

5. NIKATAE REQUEST ZIPI?

Kila dereva wa Uber/Bolt anatakiwa kuwa mwepesi kutambua mazingira na kujitoa kwenye hatari. Hata kama lengo ni kutengeneza pesa nyingi kuna safari inabidi uzikatae ili kuhakikisha usalama na amani.

Ukifika kuchukua abiria na ukaona dalili za matatizo usiwachukue. Mfano mzuri ni abiria waliolewa na kuanza kuleta fujo, au kundi kubwa la watu wakati Uber kaitisha mtu mmoja, abiria mwenye mizigo mikubwa, abiria waliochini ya umri wa miaka 18 bila msimamizi na mengine mengi.

Hautakiwi kujiweka wewe pamoja na gari lako katika hatari ya kuumizwa na kuharibiwa kisa tu safari ilikuwa ya kiasi kikubwa.

6. NI WAKATI GANI NIZIME APP YA UBER/BOLT

Kila dereva wa Uber/Bolt na majukwaaa mengine ya kusafirisha abiria anatakiwa kufahamu kuwa kupumzika ni kitu muhimu sana. Kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha unazima app yako katika nyakati zifuatazo:

  • Ukiwa umechoka: pumzika kwanza au lala kwa muda sahihi kisha uje kuendelea na kazi ukiwa fresh na mwenye nguvu mpya.
  • Wakati wa kula: Kiafya si vizuri kula kwa haraka haraka wala kuchelewa kula. Usipofata misingi sahihi unaweza kuishiwa nguvu hata mori ya kuendesha. Hakikisha unatenga muda maalumu wa kula bila usumbufu.
  • Ukienda maliwato: Zima app na umalize haja ili usikatae request.

Nini kitatokea ukikataa request za safari?

Kukataa mara chache si mbaya. Lakini ukifanya hivi mara nyingi mitambo ya Uber itagundua na utakuwa unawekwa mwishoni pale abiria wakitaka kuitisha usafiri. Kwa hiyo hakikisha unazima app unapokuwa na shughuli ya muhimu ili usiwe unakataa requests zozote.

7. NI WATEJA GANI WAZURI ZAIDI?

Kama unataka kuwa na siku nzuri katika kazi yako basi ofa usafiri kwa abiria wenye alama ya rating ya 4.8 na juu. Hii ni kwasababu hawa wamepewa alama nzuri na madereva wengine kwasababu mbali mbali kama ustaarabu, kulipa bila shida na hata kutoa motisha.

Chukua tahadhari kwa wenye alama 5.0 kwasababu mara nyingi wale watu wapya ambao wamepakua app ya Uber. Hawa huwa wanakuwa na alama hii automatically bila hata kupanda Uber.

8. ABIRIA ANATAKIWA AKAE WAPI?

Kiusalama na kisheria abiria wako anatakiwa akae kwenye siti ya nyuma. Lakini kwa maeneo yetu watu wengi hasa watu wazima huwa wamezoea kukaa mbele hivyo hutaka wakae hapo.

Siku zote unatakiwa kujitahidi kufanya wakae siti ya nyuma lakini kama watakataa na kuomba au kulazimisha wakae mbele basi unaweza kuwaruhusu.

Abiria akilazimisha kukaa mbele jaribu kuanzisha mazungumzo naye maana mnakuwa mko karibu zaidi kuliko akiwa nyuma, hivyo kukaa kimya inakua si vizuri.

9. NIRUHUSU ABIRIA KUINGIA NA CHAKULA, SIGARA AU POMBE?

Kuna watu si wastaarabu na wanaweza kuchafua gari kwa kumwaga vitu kama vinywaji, chakula na majivu ya sigara.

Wewe mwenyewe unaweza kuamua kuhusu suala hili. Kama utaona unapoteza muda mwingi sana kusafisha gari baada ya kushusha abiria wa namna hii basi unaweza kuwaomba wasifanye hivyo kwenye gari lako.

10. NISHINDANIE ABIRIA KWENYE MAENEO MAARUFU?

Kila dereva wa Uber/Bolt anafahamu yale maeneo, pamoja na ile mida ambayo ina wateja wengi. Mfano mzuri ni kama maeneo yenye Bar maarufu, uwanja wa taifa, Hoteli/restaurant kubwa, Kumbi za starehe nk.

Kwa bahati mbaya kwasababu kila dereva anayajua maeneo haya, wengi huaenda huko hivyo kuleta ushindani mkubwa na kufanya hata bei ya nauli ishuke kidogo baada ya idadi ya madereva kuzidi uhitaji wa abiria katika eneo hilo.

Pia bara bara za kuelekea maeneo haya hasa siku za mwisho wa wiki huwa na foleni kubwa kwasababu watu wengi wanaelekea huko. Hii husababisha upotezwaji wa muda mwingi sana ambao ungeweza kutumika kupata abiria wengine kwenye maeneo mengine.

Kwa hiyo ukitathmini vizuri utagundua kuwa ni bora tu kukaa kwenye maeneo uliyoyazoea ambayo una uhakika wa kupata abiria lakini pia ushindani kutoka kwa madereva wengine kwa muda huo utakuwa chini.

11. MUDA UPI NI BORA KUACHA KUENDESHA?

Suala ni kwamba, kila unapowasha gari unaingia gharama. Kila muda ambao hauna abiria kwenye gari unaingiza hasara. Badala ya kuzunguka na kuhama hama ukitafuta abiria, tafuta sehemu moja nzuri upaki gari na ulizime hadi upate abiria mwingine.

Ni muhimu sana kila dereva wa Uber/Bolt kuzingatia maswali haya ili kufanikiwa katika kazi hii. Mwisho wa siku hii ni biashara na biashara yoyote ili kufanikiwa ni lazima kipato kiwe kikubwa kuliko matumizi.

Utafanyia kazi maswali haya?

3 thoughts on “KILA DEREVA WA UBER/BOLT ANAPASWA KUJIULIZA MASWALI HAYA”

  1. Pingback: JINSI YA KUTENGENEZA PESA NYINGI KWENYE UBER/BOLT %

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *