Watu wengi huanza biashara ya kuendesha magari kwenye majukwaa ya usafiri wakidhani kwamba abiria wapo wengi muda wote na watatengeneza mamilioni haraka!. Kama haupati abiria Uber/Bolt/Linkee au kwenye jukwaa lolote lile usikate tamaa.
Hali hii ni ya muda na muda na inaweza ikawa ni kwasababu tu eneo uliopo lina madereva wengi kuliko abiria hivyo kusababisha ushindani mkubwa.
Kabla ya kuingia ndani zaidi ya jambo hili kwanza ni muhimu kufahamu aina ya madereva wanaoendesha abiria kwenye majukwaa ya Ride sharing au Ride hailing.
Madereva wa Spare time: Hawa ni madereva ambao aidha ni wanafunzi, wastaafu au watu waliokosa ajira ambao huamua tu kuendesha abiria wanapopenda au wanapopata muda kidogo.
Mara nyingi hawa huwa wapo kwenye jukwaa moja tu kama ni Uber, Bolt, Linkee au lingine. Kundi hili la madereva huwa hawachukulii udereva kama ajira ya full time bali wanapohitaji fedha.
Madereva wengine wanaoingia kwenye kundi hili ni wale wanaofanya kazi nyingine lakini wanapenda kuongeza kipato hivyo huanza kuendesha abiria baada ya kutoka kazini kwao.
Mfano kama mtu ana gari lake muda wa kutoka kazini na kurudi nyumbani badala ya kurudi na gari tupu anaona bora awashe app apate abiria hasa wanaoelekea muelekeo wa anapoishi.
Hawa pia huendesha zaidi siku za mwisho wa wiki na sikukuu kwasababu hawaendi kazini siku hizo.
Madereva wa full time: Hawa ni wale ambao wameamua kufanya biashara hii ya kusafirisha abiria kama chanzo chao kikuu cha kipato. Hawa mara nyingi wanakuwa serious zaidi, professional na mara nyingi huendesha kwenye jukwaa zaidi ya moja.
Katika siku, wiki au mwezi lazima kuna kipindi ambacho abiria wapo wengi na madereva wanapata hela nyingi na pia kuna wakati kunakuwa na ukame.
Katika makala hii utafahamu hatua za kufata ili kuhakikisha kipato chako hakishuki sana kipindi hiki
KAMA HAUPATI ABIRIA UBER/BOLT/LINKEE NK FANYA HIVI!..
1. KUBALI SAFARI ZA UMBALI MREFU NA ABIRIA WALIO MBALI NA ULIPO
Madereva wengi wanafahamu kuwa safari fupi ndio zina faida zaidi kuliko ndefu. Hii inatokana na sababu mbali mbali kama zifuatazo:
- Uwezekano wa kukwama kwenye foleni barabarani.
- Kutumia mafuta mengi kwa safari
- Kupunguza idadi ya safari kwa siku
Kwa kawaida safari fupi zinaonekana kuwa na faida zaidi pia kwasababu inafanya dereva akutane na watu wengi zaidi ambao kama wote watampa alama nzuri itafanya awe na ratings nzuri hivyo kupata kipaumbele kwenye kupata safari.
Kipindi ambacho hakuna abiria wengi sana inashauriwa kukubali safari ndefu zaidi ili kupandisha acceptance rate yako.
Sio mara zote utakapokubali safari itakubidi kupeleka abiria. Kama abiria yupo mbali sana na wewe kubali tu safari na uache yeye a kancel kama akiona hana muda wa kukusubiria.
Kitendo cha wewe kukubali abiria wa mbali na wewe na yeye kucancel kinapandisha sana acceptance rate ya dereva. Ikiwezekana unashauriwa kukubali safari kisha kumpigia abiria na kumshauri kama kuna mtu karibu aahirishe safari na wewe na achague huyo mwingine.
Hii itafanya software/mitambo ya Uber kuona kuwa account yako haibagui umbali, wewe ni dereva ambaye yupo tayari kufata abiria wa mbali pia kwako ni bora kuahirishiwa safari kuliko kuacha abiria anakosa usafiri.
Madereva wenye acceptance rate ya juu hupewa kipaumbele zaidi na Uber kuliko wale ambao hukataa safari na wateja wa mbali. Kwa hiyo hii itakuweka kwenye nafasi nzuri ya kupata safari zaidi.
2. JIUNGE KWENYE MAJUKWAA MENGINE YA RIDE SHARING
Kama haupati abiria kwenye Uber haimaanishi kuwa hautapata abiria kwenye majukwaa mengine kama Bolt, Lyft, Linkee nk.
Madereva wengi wanaofanya shughuli ya kuendesha abiria full time huwa wamejisajili kwenye zaidi ya kampuni moja.
Unapoona hakuna abiria kwenye jukwaa moja basi zima app au uende offline kisha uende online kwenye jukwaa lingine na uendelee kutengeneza pesa.
3. FANYA TAFITI YA SEHEMU ZENYE MADEREVA WACHACHE
Kwa kawaida madereva wengi hupenda kwenda kwenye maeneo yenye abiria wengi zaidi. Hii ni mbinu nzuri kwa wale wenye acceptance rate kubwa na wenye uzoefu zaidi kwenye biashara.
Hawa inakuwa rahisi zaidi kupata safari kuliko madereva wapya au wenye review za chini.
Ili kupata abiria wengi inashauriwa kutafuta sehemu ambazo hazina madereva wengi. Inaweza kuonekana kama hasara kwasababu hakuna wateja, lakini kiuhalisia ni bora kuliko kwenda kushindana na mamia ya madereva wazoefu zaidi kwenye yale maeneo yenye watu wengi sana.
4. TUMIA RAMANI KUJUA WAPI KWA KWENDA KUPATA WATEJA
Ukiangalia kwenye ramani ndani ya app yako utaweza kuona magari mengine yaliyopo online. Kwa kawaida gari likikubali safari huwa linatoweka kwenye ramani na likishamaliza safari linarudi tena kwenye ramani.
Ukiwa makini utaweza kugundua ni sehemu zipi za mji wako magari mengi yanatoweka kwenye ramani. Kama sio mbali sana basi elekea hapo maana inamaanisha kuwa kuna wateja wengi wanatokea hapo.
5. TENGENEZA PESA ZA ZIADA KWA KUALIKA MADEREVA WENGINE WAENDESHE UBER
Kama tulivyochambua katika makala hii madereva Uber wanaweza kupewa motisha ya shillingi 100,000/= kwa kila dereva mpya atakayejisajili na kuendesha safari 5 katika jukwaa hili.
Wakati hauna wateja tumia mbinu madhubuti zilizoonyeshwa kwenye makala ya hapo juu ili kuweza kupata watu wengi wajiunge na kukuingizia pesa kwenye akaunti yako.
Ukiweza kupata hata watu watano tu wapya kwa mwezi tayari unakuwa umeingiza 500,000/= tsh katika akaunti yako kutoka Uber.
Kama haupati abiria Uber/Bolt/Lyft/Moovin basi unao muda mwingi sana wa kuweza kujikita katika njia hii nyingine ya kupata pesa kuliko wale ambao wanapata wateja wengi.
5. FANYA DELIVERY ZA WAFANYABIASHARA
Moja wapo ya changamoto kubwa inayowakumba wafanyabiashara hasa wa mtandaoni ni kusafirisha bidhaa zao kwa wateja wao.
Ili kutengeneza kipato zaidi wakati hakuna abiria kwenye majukwaa ya ride sharing tafuta wafanyabiashara na utangaze huduma ya delivery kwa wateja wao.
Wateja hulipia 3,000/= tsh hadi 5,000/= tsh kuletewa bidhaa zao ndogo ndogo walipo. Ukiweza kupata bidhaa hata 20 tu kwa siku unaweza kutengeneza hadi 100,000/= kwa kutumia usafiri wako.
Unaweza kutumia uzoefu wako wa maeneo na kuhakikisha unachukua mizigo ya maeneo ya karibu karibu na ukishamaliza unaweza kuendelea na kusafirisha abiria kwa kuwasha app yako popote ulipo.
Njia rahisi ya kupata wafanyabiashara wa kuwapa namba zako wakihitaji kusafirisha ni kupitia kurasa zao za mitandao ya jamii.
Hii ni moja ya njia ambayo ukiifata vizuri utatengeneza kipato kikubwa sana na haitakusumbua kama abiria watakuwa hawapatikani Uber.
6. NENDA KWENYE MAENEO YENYE UHABA WA NAFASI ZA KUEGESHA MAGARI
Zipo sehemu nyingi sana mjini ambazo hata watu wenye magari huona bora waitishe usafiri kuliko kwenda na magari yao.
Mfano mzuri ni maeneo ya kariakoo sokoni na Posta. Watu hata wanaofanya kazi kwenye maofisi yaliyopo huko hufika maeneo haya bila magari yao kutokana na ukosefu wa parking.
Tenga siku chache ukafanye tafiti kwenye maeneo haya na uanze kuenda mara kwa mara ili kupata abiria
7. JITANGAZE / SAMBAZA VIPEPERUSHI
Katika nyanja yoyote ambazo ina ushindani mkubwa hakuna mbinu bora zaidi ya kuwashinda wengine kama kuji market.
Kuwa wakipekee, badala ya kushindania wateja kwenye jukwaa chukua muda na utengeneze vipeperushi vinavyoelezea huduma yako ya usafirishaji pamoja na mawasiliano yako.
Sehemu kuu zenye faida kubwa sana za kupeleka vipeperushi vyako ni kama zifuatazo.
A. VYUONI
Wanafunzi wengi hawana usafiri wao binafsi na ni moja ya kundi la watu ambao wanapenda sana kutoka kwenda matembezini kama beach, club nk.
Unaweza kudhani kuwa wanafunzi wa vyuo hawana hela za usafiri wa aina hii lakini si kweli. Kwanza hela wanazo pia wanapenda sana safari hasa usiku kwahiyo lazima utapata wateja tu!
Pale ambapo labda hawana data ya kuingia Uber au pale ambapo wanafunzi hawana app ya usafiri ni rahisi kukuita wewe. Au hata kama wanayo app, wakiona gari lako lipo available watakuitisha wewe sababu wanakuwa wamewahi kukuona.
B. NYUMBA ZA WAGENI
Hotels na nyumba za wageni ni maarufu sana kwa kupata abiria muda wowote. Ongea na wamiliki ili wakupe ruhusa kuweka vipeperushi kwenye reception yao. Au mpe namba za simu receptionist na wahudumu wengine ili mtu akihitaji usafiri waweze kumpa namba na umfuate.
C. HOSPITALI
Hospitali kuna abiria aina tatu, wagonjwa wanaoruhusiwa, watu wanaotoka kupeleka wagonjwa lakini pia waajiriwa kama madaktari na manesi.
Peleka vipeperushi vyako kwa waajiriwa kwasababu hawa ni rahisi kukutafuta baada ya kazi au hata kabla wakati wa kwenda. Lakini pia hawa ndio watakuwa rahisi kutoa namba zako kwa watu wengine watakao hitaji usafiri kutoka eneo husika.
Endelea kujenga mahusiano mazuri hasa na hawa wafanya kazi ili kuhakikisha kuwa wanakutafuta wewe tu hata kwa safari zao nyingine za nje ya kazini au hata kusafirisha wagonjwa pale ambapo usafiri wa hospitali unaposhindikana.
D. MALLS
Haya ni majengo yenye mkusanyiko wa maduka na biashara za aina nyingi kwenye eneo moja. Maeneo haya kwa kawaida huwa yanafurika watu kutokana na umaarufu wa biashara na huduma zinazotolewa.
Mfano wa mall ni kama Mlimani city mall, Aura mall, Dar free market, GSM mall, palm village mall nk. Unaweza kwenda na kusambaza vipeperushi kwa watu , kwenye biashara au maeneo yanayozunguka majengo hayo.
Kama haupati abiria Uber au kwenye jukwaa lolote la ride sharing/hailing hakikisha haikukatishi tamaa. Jaribu mbinu hizi na bila shaka lazima utapandisha kipato chako tena.
Tafadhali tushirikishe kwenye comments mbinu zako ya kuongeza kipato pale abiria wanapopungua kwenye jukwaa unaloendeshea abiria.
Pingback: MADEREVA WA LINKEE TANZANIA WANAPATA FAIDA HIZI -
Ahsante sana kwa dondoo hii ila marekebisho ya nauli zinatuumiza
Mimi kiunumla huwa nashindwa kuelewa ninawenisiaccept safari moja unakuta umeshushwa rates kama mbili hivi ,na ninaweza nikafanya safari kama nne mfululizo unaweza kukuta imepanda eidha moja tu kwanini?