JINSI YA KUPUNGUZA GHARAMA YA MAFUTA YA GARI

Mafuta ndio mtaji na gharama kubwa kwa madereva wa majukwaa yote ya usafirishaji wa abiria. Hata ukitengeneza fedha nyingi kiasi gani unatakiwa kutoa gharama ya mafuta ndio ubaki na faida.

Kwasababu ya hili, ili kupata faida kubwa ni lazima dereva ufahamu jinsi ya kupunguza gharama na kuongeza kipato.

JINSI YA KUPUNGUZA GHARAMA YA MAFUTA KWA MADEREVA

Kwanza kabisa tunatumaini kuwa unafahamu kuwa kuna aina za magari zinatumia mafuta mengi kuliko aina nyingine. Mfano mzuri wa magari yanayotumia mafuta kidogo zaidi ni Toyota IST.

Bila shaka hii ndio sababu kuu ya kuongezeka kwa aina hii ya magari Tanzania na Afrika nzima. Hivyo kabla hatujaanza na mbinu nyingine, ni muhimu kuhakikisha au kufanya uwezalo kupata aina sahihi ya gari ili kuokoa gharama hii.

SOMA: Magari yanayokubaliwa kusajiliwa Uber Tanzania.

1. PUNGUZA KASI

Unapoongeza spidi ya gari ndivyo gari hutumia mafuta mengi zaidi kuliko unapoendesha taratibu. Tafiti zinaonesha kuwa kupunguza kasi ya gari kutoka 128 kph hadi 112 kph na 96 kph kunapunguza kiasi cha mafuta kutumika kwa 10%-25%.

Madereva wengi wanapenda kwenda haraka kwasababu ya kumaliza safari kulipwa na kuchukua abiria wengine. Hii inaweza kuwa sawa lakini kwa kuokoa mafuta ni bora kutoendesha kwa kasi.

Hii ndio njia ya kwanza na rahisi zaidi katika njia 8 tutakazoenda kukuonesha katika makala hii.

2. ZINGATIA UBORA WA GARI

Kuwa makini katika utunzaji wa gari lako ni njia ya pili bora zaidi ya kupunguza gharama ya mafuta. Gari ambalo linafanyiwa marekebisho mara kwa mara kama kuhakikisha uwepo wa mafuta ya engine, maji, filter ya hewa nk huwa linaokoa 15% ya gharama za mafuta.

Magari mabovu huhitaji nguvu zaidi ya injini kuyaendesha hivyo kusababisha mafuta mengi zaidi kutumika kuliko magari yaliyo kwenye hali nzuri.

3. ZINGATIA UBORA WA MATAIRI

Kama ambavyo tayari unafahamu matairi ndio yanabeba uzito wa gari na kuyagusisha na barabara. Yakiwa na ubora mzuri kwanza huhakikisha usalama, pili husaidia gari liende vizuri na kiwepesi.

Matairi mabaya na yasiyokuwa na upepo wa kutosha hupunguza ufanisi wa gari hivyo hufanya gari litumie 3% zaidi katika mafuta ili kufidia pungufu hilo la ufanisi.

Hivyo ili kuokoa mafuta hakikisha matairi yote manne yana upepo wa kutosha na yapo katika hali nzuri wakati wote.

4. PUNGUZA UZITO WA GARI

Gari zito linahitaji mafuta mengi zaidi kuliendesha, zipo njia nne unazoweza kutumia kuhakikisha uzito wa gari hauathiri kiasi cha mafuta yaliyopo.

  • Tumia gari jepesi: Wakati wa kununua gari au kuchagua gari kutoka kwa mmiliki hakikisha unachagua gari jepesi kuliko zito. Zipo njia nyingi za kujua uzito wa model zote za magari, fanya utafiti ufahamu kabla ya kuanza kuendesha.
  • Ondoa mizigo ndani ya gari: Punguza vitu vizito kwenye gari visivyo na ulazima wa kuwepo kama matairi zaidi ya moja au tumia gari zisizokuwa na zile carrier nzito za kuweka mizigo juu.
  • Usibebe abiria wenye mizigo mizito: Moja ya malalamiko ya madereva wengi ni kufata abiria na kukuta wametoka kwenye manunuzi na kutaka kusafirishwa na mizigo mizito. Hakikisha abiria analipia mzigo kama mabasi na daladala yanavyolipisha mizigo.
  • Usijaze mafuta Full tank: Lita 50 za petrol zina uzito wa 37 kg, hizi zitafanya mafuta mengi yatumike sababu uzito wa gari umeongezeka. Badala yake bora kuweka nusu tanki na kuendelea kuongeza yanapokaribia kuisha.

5. TUMIA GIA KIUSAHIHI

Kama unaendesha gari la manual unaweza kupunguza matumizi ya mafuta kwa kuhakikisha unabadilisha gia ipasavyo.

Madereva wengi husubiri hadi injini itoe ule mlio mkubwa wa kuzidiwa pale mwendo unapozidi gia ndipo wabadilishe. Hii inasababisha mafuta yatumike mengi bila kuongezeka kwa kasi ya gari.

Hakikisha unabadili gia mara tu unapohitaji kuongeza mwendo.

6. ENDESHA TARATIBU KWENYE MATUTA

Majaribio yanaonesha kuwa kuendesha kwenye matuta katika kasi ya taratibu huokoa mafuta kuliko kuendesha kwa kasi na kukanyaga brake ghafla pale pale kwenye tuta kisha kuondoka kwa spidi kubwa tena.

Ukipunguza kasi katika umbali mdogo kabla ya tuta na ukapita kwa mwendo huo huo halafu ndio ukaongeza kasi taratibu baada ya kupita tuta utakuwa unaokoa mafuta na pia kutunza ubora wa gari lako.

7. PUNGUZA MATUMIZI YA KIYOYOZI

Kila dereva anafahamu kuwa Air conditioner inatumia mafuta sana. Lakini ukweli ni kwamba si vizuri kuendesha abiria maeneo yenye joto kali bila kuwawashia kiyoyozi. Usipowasha abiria wanaweza kulalamika na kutoa alama mbaya kwenye akaunti ya dereva katika jukwaa la usafiri.

Kwa hiyo suluhisho la hii si kuzima kabisa bali kuzima pale ambapo hauna abiria kwenye gari. Ukiwa peke yako hakikisha unafungua madirisha au kama umeegesha gari ni bora kutoka na kukaa nje upate upepo kuliko kusubiri ndani ya gari na kuwasha kiyoyozi.

8. NUNUA MAFUTA KWENYE VITUO VYENYE BEI NDOGO

Unaweza kuona kama tofauti ya bei ni ndogo sana kutoka kwenye muuzaji mmoja kwenda kwa mwingine. Lakini ukifikiria kwa mwezi au kwa mwaka unanunua mafuta mara ngapi na kiasi gani basi utaona kuwa unaokoa hela nyingi tu mwisho wa siku.

Mafuta ndio gharama kubwa zaidi kwa dereva yoyote katika sekta ya usafirishaji abiria. Ukifahamu jinsi ya kupunguza gharama hii utaweza kuongeza kiasi kinachobaki baada ya kumaliza shift yako ya siku ya kuendesha abiria.

Ni vizuri kuanza na njia unazoweza kuzimudu kwanza kisha kuendelea na njia nyingine tulizoongelea kwenye makala hiii. Muhimu kuliko yote ni kuchagua magari yaliyoundwa kutumia mafuta kidogo.

Je, umejifunza mbinu yoyote mpya kupitia makala hii? Tushirikishe mbinu zako za kupunguza gharama ya mafuta ya gari ili madereva wengine waweze kujifunza kutoka kwako.

1 thought on “JINSI YA KUPUNGUZA GHARAMA YA MAFUTA YA GARI”

  1. Pingback: ONGEZEKO LA NAULI UBER: MAANA NA TAHADHARI -

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *