Jinsi ya kupata 5 strars

JINSI YA KUPATA 5 STAR RATINGS KWA MADEREVA WA TEKSI MTANDAO

Katika makala hii tumeamua kuchambua jinsi ya kupata 5 stars na reviews kwa ajili ya madereva wa teksi mtandao kwasababu hiki ni kigezo kikubwa cha kupata abiria kwa wingi zaidi.

Majukwaa ya usafiri wa teksi mtandao kama Uber, Bolt, Ping, Paisha, Little ride, Indriver and nyinginezo yameweka system ya madereva kupewa alama na abiria kwasababu yanataka ubora wa hali ya juu katika huduma zao.

Baada ya kukamilika kwa kila safari abiria anaweza kumpa alama dereva kutokana na huduma aliyopokea. Pia dereva anaweza kumpa alama abiria kutokana na safari ilivyoenda kati yao.

Alama zipi ni mbaya kwa dereva?

Kwenye majukwa mengi kama dereva atapata alama chini ya nyota 4.6 basi atakuwa kwenye hatari ya kupoteza akaunti yake ya udereva.

Kila dereva anavyojisajili na kukubaliwa kuanza kuendesha abiria huwa anapewa nyota 5 (5 stars automatically). Unavyozidi kuendesha alama zako unazopewa na abiria wako hujumlishwa na kugawanywa kisha kubadilika ipasavyo.

Kwasababu sekta hii inatumia teknolojia za hali ya juu, makampuni huwa yanafahamu madereva gani wanapendwa sana na hivyo kutoa fursa za safari zaidi kwa hao madereva wenye alama za juu zaidi kuliko wenye alama za chini.

Kutokana na hili, ni muhimu sana kwa kila dereva kuhakikisha alama yake haishuki 4.6 ili kupata mafanikio makubwa zaidi kwenye biashara hii ya kusafirisha abiria.

Jinsi ya kupata 5 stars nyingi kutoka kwa abiria.

1. KUWA DEREVA MZURI

Unapokubaliwa ombi lako la kuendesha abiria kwenye majukwaa ya Teksi mtandao inamaanisha kuwa wewe ni dereva mzuri. Hii ni kwasababu majukwaa yote ya usafiri wa aina hii hukubali madereva wenye vigezo vinavyotakiwa kwa ajiri ya kutoa huduma bora kwa abiria.

Abiria anapopanda gari la dereva anategemea kuwa madereva wote ni makini na wenye ujuzi wa hali ya juu. Hivyo unatakiwa kuhakikishia kuwa ni kweli wewe umekidhi viwango kwa kufata misingi ifuatayo.

  • Heshimu alama za barabarani.
  • Endesha vizuri na kwa umakini siyo kukanyaga breki ghafla sentimita moja kabla ya tuta au shimo.
  • Acha nafasi ya kutosha kati yako na gari la mbele yako.
  • Kuwa makini na barabara pamoja na watembea kwa miguu. Macho yawe barabarani muda wote na sio kwenye simu tu.
  • Overtake panapostahili na kwa umakini.
  • Tumia ishara sahihi kabla ya kuchukua hatua kama kuwasha indicator kabla ya kukata kona.
  • Kuwa mvumilivu na mstaarabu na madereva wenzako, usipige honi bila misingi wala usitupiane maneno ya ubishi na madereva wengine hata kama wao wana makosa.

Kila mtu anapenda kusafiri kwa amani kwa hiyo ukiendesha vizuri lazima abiria wako watafurahia na watapenda kukupa alama kubwa.

2. FATA MISINGI YA HUDUMA KWA WATEJA

Gari lako ndio ofisi yako, abiria wanapoingia wanategemewa kuhudumiwa vizuri kama customer care wa makampuni wengine wanavyohudumia wateja.

Fahamu misingi yote ya kutoa huduma kwa wateja na ufurahie alama kubwa kutoka kwa abiria wako wote!

SOMA: Misingi ya huduma kwa wateja kwa madereva Uber/Bolt/ Linkee nk

3. FAHAMU NJIA NZURI NA MAENEO MAARUFU

Moja ya sifa ya dereva mzuri ni kufahamu maeneo mengi katika mji anaofanyia shughuli. Maeneo kama uwanja wa ndege, vituo vya mabasi ya mikoani, sehemu za kitalii, mahoteli makubwa, maofisi makubwa nk huwa yanatembelewa na watu wengi sana.

Jitahidi kufahamu maeneo mengi na njia mbalimbali za kufikia maeneo hayo kwa haraka zaidi. Unaweza kuwa haufahamu maeneo mengi mwanzoni lakini baada ya muda utapata ufahamu zaidi kupitia kupeleka abiria mbali mbali.

Ukipata njia za mkato, au njia zisizokuwa na taa nyingi sana ambazo ni za haraka basi utafurahisha sana abiria maana wengi huwa wanakuwa na haraka.

4. HUDUMA ZA ZIADA

Kuwa dereva sio tu kukaa kwenye gari na kuendesha abiria. Fanya zaidi kwa kusaidia abiria wako na huduma za ziada kama chaja za simu, saidia abiria kuingia kwenye gari kama wanapata shida labda kwa kuumia au ulemavu.

Kama wamechelewa kidogo kufika kwenye eneo la kuwapakia basi wapigie simu halafu wasubiri kidogo. Pia kama wanaelekea eneo ambalo hawalifahamu sana unaweza kuwasaidia kwa kuwaelekeza kidogo wajue angalau pa kuingilia na kutokea.

Hivi vyote ukifanyia abiria lazima wakupe 5 stars kwasababu wewe unaweza kuona umefanya kitu kidogo kumbe kwao wameona kama umewasaidia sana.

5. JITOLEE KAMA TOUR GUIDE

Kama unaendesha kweye jiji ambalo lina majengo au vitu vizuri vya kitalii basi usisite kuwaelezea abiria ambao wamepaona kwa mara ya kwanza.

Ukipata muda jaribu kujifunza kuhusu maeneo , majengo au vitu maarufu katika mji wako ili uweze kuwagusa abiria wako wageni utakaowapata.

6. FAHAMU JINSI YA KUTUMIA GPS

Kuna wakati gps huwa zinakosea na kufanya mtu uzunguke eneo moja bila sababu ya msingi. Hii hutokea hasa pale ambapo barabara uliyopo ina foleni kubwa na gps inajaribu kukuonesha njia nyingine yenye unafuu zaidi.

Kama tayari una uzoefu na barabara husika basi unaweza kutofata gps na kuchagua njia bora zaidi. Baadaye gps itajiweka sawa yenyewe na kuendelea na njia uliyoichagua.

Ukifanya hivi utaonesha abiria wako kuwa wewe ni dereva mzuri na unajali kuwafikisha kwa muda mfupi.

7. KUWA MSTAARABU

Kila mtu anapenda mtoa huduma mchangamfu, mstaarabu na mweye wema. Weka kuchoka na hasira pembeni muda wote na upokee abiria wako kwa uchangamfu.

Salamu wakati wa kuonana na wa kuagana pia ni muhimu sana kwa kila abiria unayemsafirisha. Watakie mema wanapoondoka kwa kuwaambia kazi njema kama wanaenda kazini au safari njema kama umewapeleka stendi au uwanja wa ndege.

Hii itasaida abiria wafurahishwe na wema wako na waguswe kukupa 5 stars.

8. USIONGEE SANA WALA USIKAE KIMYA SANA

Unapokutana na abiria wako katika kuwasalimia tu unaweza kufahamu kama ni watu waongeaji au sio waongeaji.

Usiwe mkimya sana ukiona abiria anakuongelesha mara kwa mara. Utafahamu kama abiria anapendelea kuongea na wewe pale atakapokuwa anakuuliza maswali mengi.

Kama wewe haujisikii kuongea sana si mbaya, basi unaweza kutoa salamu vizuri, kujitambulisha kisha kukaribisha tu. Mara nyingi abiria hupendelea kujikita kwenye simu zao kuliko kuongea sana.

9. USAFI WA GARI

Watu wengi sana wanapenda usafi na harufu nzuri. Kama ambavyo tumesema mara nyingi katika blog yetu, wewe kama dereva gari lako ndiyo ofisi yako.

N i muhimu sana kuhakikisha linakuwa safi kila unapochukua abiria mpya. Haiwezekani kusafisha nje kila baada ya kushusha abiria, hapa tunaongelea usafi wa ndani ya gari kwanza.

Hakikisha vitu vilivyopo ndani mfano charger za simu vimepangwa vizuri, ondoa uchafu kama makopo na pia weka air freshner ina harufu nzuri ya kuvutia.

Moja ya njia za kuhakikisha gari lako linakuwa safi wakati wote ni kuepuka kula vyakula hasa vyenye harufu kali ndani ya gari. Pia kutoa mchanga kwenye mazulia hasa baada ya kusafirisha abiria wanaotokea maeneo yenye mchanga mfano ufukweni.

10. OMBA REVIEW

Mara nyingi sana abiria huwa na haraka hivyo kusahau kutoa alama na kuacha comment juu ya dereva. Hii inaweza kukukosesha review nzuri kutoka kwa abiria ambao kiukweli wamefurahia sana huduma.

Ukizingatia kuwa wale abiria wenye matatizo ni wepesi kutoa alama mbaya wasiporidhika, ni muhimu sana kuwakumbusha abiria ambao mmeongea vizuri wakuwekee alama.

Usishawishi au kulazimisha abiria akupe stars. Badala yake toa huduma bora na kisha waambie kuwa unatumaini wamefurahia huduma na kama wamefurahia basi waisahau kukupa alama.

Abiria wakijua kuwa itakusaidia sana kupata alama nzuri kutoka kwao wataguswa kukuachia review nzuri kwenye akaunti yako.

Sasa unafahamu jinsi ya kupata 5 stars kwenye akaunti yako ya dereva katika jukwaa lako la usafirishaji. Je, mbinu ipi umeifurahia zaidi kati ya hizi?

Kumbuka kuwa hauwezi kufurahisha kila mtu. Wapo ambao watakuwa na uungwana na watakupa alama nzuri, pia wapo ambao watakuwa wagumu na watakupa alama mbaya hata iweje.

Jikite zaidi katika kuboresha huduma yako ili kupata alama nzuri zaidi badala ya kuumizwa au kuwa na hofu sana na wale wanaotoa alama mbaya.

SOMA: Kila dereva Uber/ Bolt lazima awe na vifaa hivi

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *