Baada ya jukwaa kinara wa huduma za teksi mtandao duniani Uber kusitisha huduma zake nchini, ikifuatiwa na Bolt ambao waliondoa huduma ya usafiri wa gari kwa watu binafsi na kuielekeza kwa wateja wa makampuni huku chanzo kikitajwa kuwa ni LATRA kuzitaka kampuni hizo kupunguza asilimia za makato kwa dereva mpaka kufikia asilimia 15.
Kufatia mazungumzo baina ya LATRA, kampuni za Uber na Bolt na wadau wengine wa teksi mtandao, kampuni hizo ziliridhia kurejesha huduma zao nchini. Hizi zikawa habari njema kwa watumiaji wa teksi mtandao. Lakini, je?, kufungwa kwa majukwaa haya nchini kumewaathiri kwa kiasi gani wamiliki wa magari ambao walikuwa wakishiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha utoaji huduma kwenye majukwa haya.
SOMA ZAIDI: Kwa nini baadhi ya madereva wa teksi mtandao hawa ‘start trip’ wanapowabeba abiria?
Timu ya Weibak imefanya mazungumzo na baadhi ya wamiliki wa magari ambao magari yao yalikuwa yakitumika katika majukwaa haya kutoa huduma, kutaka kufahamu ni kwa namna gani kusitishwa kwa huduma kwenye majukwaa haya vinara kumeyaathiri maisha yao ya kila siku na kujua matarajio yao kuelekea kurejeshwa kwa huduma hizo.
Imran Shakur, mmiliki na dereva wa gari anasema “Nililazimika kuchukua mkopo Kwenye tasisi ya fedha (Bank) ili kuongezea kununua gari la biashara na kujiunga na Bolt. Lakini, nimefanya kazi kwa miezi mitatu pekee na kupokea taarifa juu kupunguzwa kwa magari(Bolt). Licha ya kupambana kulipa mkopo lakini bado biashara ya teksi nje ya kampuni hizo (za teksi mtandao) ni ngumu. Haiaminiki”.
Upepo huu haukumpitia Shakur pekee, Ashura Jumanne, mama wa watoto sita, aliachiwa magari matatu na mumewe (marehemu) miaka mitatu iliyopita. Kwa kiasi kikubwa, maisha yake yalitegemea zaidi kipato alichokuwa anakipata kupitia magari yake yaliyokuwa yakitoa huduma ya usafiri kupitia teksi mtandao. Ashura anaamini kufungwa kwa Uber na kutolewa kwa huduma ya magari kwenye Bolt kumemfanya kupoteza kipato alichokuwa anakipata awali.
SOMA ZAIDI: Mbinu za Kukusaidia Dereva wa Teksi Mtandao Kutengeneza Faida Kwenye Pesa Unayoingiza
“Biashara ya usafirishaji abiria kwa njia ya magari binafsi (bila teksi mtandao) ni ngumu kwa sababu wateja wengi hawaamini usalama wao kwenye magari yasiyokuwa kwenye mfumo wa utambuzi kama Bolt, Uber au Ping kutokana na sababu za kiusalama , unaweza kupata wateja Kama sita mpaka tisa kwa wiki kitu ambacho ni kigumu kulipa madereva, mafuta na kupata faida”. Alisema Ashura.
Mkwamo huu haukuishia kuwaathiri wamiliki tu, bali hata madereva waliokuwa wanaendesha magari ya wamiliki hawa walianza kupoteza kazi zao.
“Japo nilibahatika kubaki katika Kampuni ya Bolt ambapo nina magari mawili katika kampuni hiyo lakini bado magari mengine kadhaa nimeamua kuyapaki. Naendelea kupambana ili kujiunga na Kampuni mpya za Ping na Paisha. Japo bado masoko yake na maslahi si makubwa Kama ilivyokuwa kwa Uber na Bolt” alisema Gharib Mohamed.
Gharib anachukulia kurejeshwa kwa huduma ya usafiri wa gari kwenye Bolt kama fursa itakayomsaidia kuinuka tena kiuchumi. Lakini mashaka yake yanabaki kwenye ubora wa huduma za majukwaa haya kama ilivyokuwa awali.
“Japo wanarejea ila ubora wao utapungua kutokana na kuongezeka kwa makampuni mapya Kama Ping ambayo yanazidi kupata umaarufu na kuleta ushindani mkubwa kwa Uber na Bolt”. Gharib aliongeza.
Hatua ya Uber kutaka kurejesha tena huduma zake nchini, na Bolt kurejesha usafiri wa gari kwa watu binafsi inaonekana kufurahiwa na wamiliki wengi wa magari. Tofauti pekee iliyopo kwa sasa, ni kuwa wamiliki hawa wa magari wanahitaji kujengewa upya imani ya kufanya kazi na majukwaa haya kama ilivyokuwa awali.
“Wahusika wote kuanzia LATRA na Kampuni ya Bolt wanapaswa kuweka makubaliano ya muda mrefu na ya wazi ili watu warudi kuwaamini na kufanya nao biashara tena”. Alisema Ashura Jumanne, mmliki wa magari.
Pia, kukosekana kwa abiria katika majukwaa ya teksi mtandao yaliyokuja baada ya Uber na Bolt ni changamoto nyingine inayotajwa na wamiliki wa magari kama sababu ya kuendelea kuwaingizia hasara wanapojaribu kuyatumia majukwaa hayo kama mbadala.
SOMA ZAIDI: Je, dereva unajihisi kunyonywa na majukwaa ya teksi mtandao?
Masoud Mussa, mkazi wa Temeke anasema “Ilinichukua siku 4 kupata wateja watatu tuu kupitia kampuni za Paisha na Ping. Nilianza kuzitumia Kama mbadala (baada ya) Uber na Bolt kupunguza na kusitisha hudama zake. Idadi ndogo kabisa ya wateja kuwahi kuipata tangu nianze biashara ya teksi kwa njia ya mtandao miaka mitatu iliyopita”.
Kwa upande wake Hashim Sadala, mmiliki na dereva wa gari, anadhani kampuni changa za majukwaa ya teksi mtandao zinapaswa kufanyiwa marekebisho kama sehemu ya kuboresha huduma zao.
Pamoja na majukwaa mapya kudaiwa kuwa na watumiaji wachache, lakini kwa Hashim, kampuni hizo mpya ni kama mbadala sahihi utakaopunguza migogoro kati ya madereva na wamiliki wa vyombo vya moto.
“Kuwepo kwa watanzania kwenye umiliki wa biashara hii itatusaidia sana kwetu madereva kueleweka tunapodai haki zetu kuliko wageni”.
Hashim Sadala, dereva na mmliki wa gari.