Hivi karibuni tumeweza kushudia Kampuni kubwa duniani inayojihusisha na huduma za taksi mtandao, Uber, ikisimamisha shughuli zake nchini. Baadae kidogo, Bolt nao wakasitisha huduma ya usafiri wa gari kwa watu binafsi, na badala yake huduma hiyo ikaelekezwa kwa makampuni.
Kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Bolt, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ikatoa tamko kuwataka abiria waendelee kutumia huduma nyingine za taksi mtandao zikiwemo Ping, Littleride na Paisha.
Lakini, Je, unazifahamu programu hizi zinazotoa huduma ya taksi mtandao nchini?
Lukelo Francis ni mwandishi wa habari kutoka jijini Dar es Salaam. Pamoja na kukiri kutumia huduma za taksi mtandao katika shughuli zake, Lukelo anasema hakuwahi kutumia programu za taksi mtandao tofauti na Uber na Bolt.
“Ndio nafahamu kwamba kuna programu nyingine tofauti na Uber na Bolt ambazo zinatoa hizi huduma (taksi mtandao). Kwa mfano, kuna hii InDriver, kuna Paisha, lakini pia kuna programu nyingine ambazo ni za watanzania naona zinatangazwa, lakini mimi sijawahi kuzitumia. Lakini nafahamu kwamba zipo na zinafanya kazi”. Lukelo anasema.
Baada ya Uber kusitisha huduma zake nchini, na Bolt kusitisha huduma ya usafiri wa magari kwa watu binafsi. Lukelo analazimika kuanza kujaribu kutumia programu nyingine zinazotoa huduma za taksi mtandao. Lakini bado anakosa imani na programu hizi mpya kwake.
“Bila shaka, ninawaza kuzitumia lakini mpaka sasa bado sijaanza kuzitumia. Na moja ya sababu ambazo zimefanya mpaka hivi sasa sijazitumia ni kuwa bado sijaamini kama zinafanya kazi vizuri. Hasa ninaposikia kuwa hii hapa(programu ya taksi mtandao) ni ya mtanzania nashindwa kuamini kama itakuwa inafanya kazi vizuri, sijaamini kama kuna madereva ambao wanazitumia kufanya nao kazi”. Lukelo aliongeza.
Cleopatra Ngesi ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye pia hutumia huduma za taksi mtandao wakati anakwenda chuoni na hata anaporejea nyumbani Tabata. Kwa Cleoptra, hakuna programu nyingine tofauti na Uber na Bolt ambazo humjia kichwani mwake kila wakati anapotaka kusafiri.
Cleopatra anasema “Kwa programu nyingine kusema kweli sizifahamu sana kama ninavyozifahamu hizi mbili (Uber na Bolt), kuna programu (za taksi mtandao) nilikuwa naziona kwenye simu yangu, lakini sikuweza kuzizingatia sana kwa sababu nilikuwa najua kuna Bolt na Uber”.
Hata hivyo, suala la kutokuzingatiwa kwa programu hizi za taksi mtandao (tofauti na Uber na Bolt) linaonekana kuwaathiri madereva wa taksi mtandao hasa katika kufanya chaguzi za programu watakazotumia kutoa huduma za taksi mtandao.
Moses Filbert, dereva anayetumia zaidi programu ya Bolt kutoa huduma za taksi mtanadao anasema “Nadhani wengi hawapendi programu nyingine, japokuwa wanazi ‘promote’ kwa kiasi kikubwa. Lakini bado hazijawa na wateja wengi sana kama ilivyo kwa Bolt”.
“Wakizi ‘promote’ vizuri kwa abiria wakazielewa, itakuwa ni rahisi zaidi kwa sisi madereva kuweza kuzitumia zaidi”. Moses aliongeza.
Kama ilivyo kwa Moses, Cleopatra naye anaamini kuwa wamiliki wa programu za taksi mtandao kama vile Paisha, Littleride, Ping na nyinginezo, bado wana safari ndefu katika kuwafanya abiria na watumiaji wa taksi mtandao ‘kuuzingatia’ uwepo wao.
“Mimi naona hizo kampuni ziji ‘promote’ maana Bolt niliona wamejitahidi, na Uber wakawa wanatoa matangazo ndio maana tukawajua. Halafu pia huduma zao (Bolt) zilikuwa nafuu”. Anasema Cleopatra.
Pamoja na kujitangaza kwa kampuni hizi pamoja na kutoa huduma kwa bei nafuu, Lukelo Francis anadhani kuwa mafanikio ya taksi mtandao, kwa kiasi kikubwa yanachagizwa na ubora wa huduma wanazo zitoa.
“Tatizo lililopo ni kwamba sina imani nazo, kwa hiyo ambacho kinaweza kufanyika hapo ni kutoa huduma nzuri. Unajua kitu kizuri kinajitembeza chenyewe kwamba huyu atamwambia mwenzake kwamba ‘wale jamaa wako vizuri’ Kwa hiyo, ni kutoa tu huduma nzuri kama ilivyokua kwa Uber na Bolt na bila shaka watapata wateja”. Lukelo anasema.
Napenda darasa lako sana mkuu
Tunafurahi kusikia hivyo Bruno.
Naomba ushauli nafanya taxi mtandao kwasiku naweza pata elfu 35 mpaka 40 nikitoa pesa ya mafuta elfu 17 kiasi kinachobakia napeleka nyumbani shidaipo apa endapo gari litasumbua nakosa pesa ya matengenezo nifanye vipi ilinipate pesa ya matengenezo endapo litasumbua ?
Hili ni swali zuri sana Bruno na linaweza likawa ni changamoto kwa wengi. Kwanza unatakiwa kufahamu kwamba kila biashara ina gharama za uendeshaji. Gharama hizi zinaweza kuwa zinatokea kila siku kwa mfano mafuta. Gharama zingine zinaweza kuwa za mara moja kwa msimu fulani kama vile service ya gari kila baada ya kilomita kadha. Lakini pia kuna gharama zingine hutokea kwa dharura kama vile matengenezo endapo gari litasumbua.Uzuri ni kwamba hizi gharama zote unazokumbana nazo unaweza ukazitambua mapema na ukaziwekea mkakati ili hata zikitokea kwa kushitukiza uwe umejianda.
Njia ya uhakika kabisa ambayo una shauriwa kufuata baada ya kuzitambua gharama zote zinazohusika na biashara yako. Ni kuhakikisha kwamba unatenga asilimia fulani ya kipato chako kwa ajili ya kugharamikia biashara yako na kiasi kingine unakichukua kwa matumizi yako binafsi ili maisha yaweze kwenda vizuri.Katika kutenga asilimia za kipato chako hakikisha unatenga asilimia ambayo haitaathiri kwa upande mwingine maisha yako lakini kwa upande mwingine kiwe cha kutosha kutocheleza gharama unazokumbana nazo mara kwa mara kwenyye biashara yako. Hii itakusaidia hata katika kuepuka kuchukua pesa ambazo hazikuwa kwenye hesabu zako kama vile kukopa.
Lini mtarudi tufanye kazi naona maneno mengi rudini tufanye kazi asietaka aturie watakao penda wayafa