Kwanza kabisa ni vizuri kufahamu na kukumbuka kwamba Uber kusitisha huduma Tanzania ni maamuzi ya ghafla tu kutokana na mabadiliko ya ada yaliyopitishwa na LATRA kuanzia Aprili 2022.
Kampuni imeshatoa tamko kuwa inaendelea kuwasiliana na wadau ikiwemo uongozi wa LATRA ili kuona kama kuna uwezekano wa kufikia muafaka mzuri utakaowawezesha kuendelea na biashara.
Kwa hiyo bado kuna uwezekano wa kampuni kurudi na madereva kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Kama wewe ulikuwa unatengeneza kipato kupitia kampuni hii, basi fata dondoo zifuatazo ili kuhakikisha unaendelea kutengeneza pesa vizuri tu hata kama kampuni haipo.
1. Pata Updates kutoka Uber
Kwasababu uongozi ulitoa tamko kuwa kusitishwa kunaweza kuwa kwa muda mfupi hadi muafaka utakapofikiwa, ni vizuri kujitahidi kufatilia taarifa kupitia tovuti ya kampuni, magazeti, radio na hata T.v. Watakapoamua kuendeleza huduma, watu wa kwanza watakaotaka wafahamu ni madereva maana abiria siku zote wapo wengi tu.
Kwa mfano kampuni ya Bolt ambayo nayo ilitangaza kuwa ingesitisha baadhi ya huduma, ilikutana na waandishi wa habari na kutoa tamko kuwa wamefikia muafaka mzuri na LATRA. Kwa hiyo madereva wote pamoja na abiria walifahamishwa kuwa huduma zitaendela bila shida.
Hii inaonesha kuwa upo uwezekano wa makampuni haya kujadiliana na mamlaka na kuomba kulegezewa masharti kidogo. Kwa hiyo hakikisha unafatilia habari ili usikose taarifa mpya.
2. Ungana na madereva wengine
Njia nyingine rahisi ya kupata taarifa mpya haraka ni kuwa karibu na madereva. Ukiachana na hili la taarifa, madereva wengine wanaweza kukupa ushauri mzuri zaidi kuhusu jinsi ya kutengeneza pesa kwa kupitia kujiunga na makampuni mengine au vyovyote vile.
Umoja na mshikamano ni muhimu sana katika kazi kama hizi. Ndio maana sisi Weibak tuliamua kuanzisha group la FaceBook kwa ajili ya madereva wa programu za safari.
Lengo kubwa limekuwa kuwaweka madereva karibu ili kubadilishana mawazo na pia kujifunza. Sekta hii ya programu za usafiri bado inakua Tanzania, changamoto zipo nyingi lakini tunaamini mabadiliko yanawezekana.
Bonyeza HAPA kujiunga kwenye group la madereva ! Karibu sana!
3. Endesha kwenye majukwaa mengine
Watu wengi hawafahamu hili lakini Tanzania kuna makampuni mengi tu ya programu za safari. Kampuni moja kusitisha huduma haitakiwi kumyumbisha sana dereva kwasababu unaweza kujiandikisha na kuanza kazi kwenye kampuni nyingine chap chap!
Kama tayari umekuwa ukiendesha kampuni zaidi ya moja basi si mbaya kujaribu na nyingine ili kuziba pengo la hii iliyosimamisha huduma.
Hakikisha unafanya uchunguzi wako kabla ya kujisajili kwenye kampuni nyingine. Unaweza kutembelea tovuti zao kuona sheria zao au kutembelea kurasa zao za mitandao ya kijamii kuona wateja wao wanasemaje.
Njia bora zaidi ni kuwasiliana na madereva wengine wanaofanya kazi kwenye programu hizo na kuwauliza mtazamo wao kuhusu kampuni husika na kama inakufaa.
Unaweza kujiunga kwenye group la Weibak la madereva ili kutafuta madereva hawa na kupata majibu haraka!
4. Wasiliana na abiria wako wa zamani
Kama wewe ni dereva mzuri basi lazima utakuwa na namba nyingi za simu za abiria waliofurahia huduma yako. Kumbuka kuwa Uber kusitisha huduma Tanzania hakujasumbua madereva tu bali na abiria pia.
Wapo abiria ambao kutokana na sababu moja au nyingine wanaamini sana huduma za kampuni hii kuliko nyingine. Kwa hiyo abiria hawa wanaweza kufurahia ukiwaarifu kuwa upo na wakihitaji usafiri wakutafute tu kwa simu ili uendelee kuwapa huduma vile vile kama mwanzo.
5. Tafuta kazi ya udereva
Zipo fursa nyingine nyingi tu kwa ajili ya madereva ambazo unaweza kufanya part time au full time na ukapata kipato kizuri. Unaweza kupata fursa hizi kwa kuchangamkia ajira au tenda kwa njia zifuatazo.
- Ulizia kazi: wasiliana na watu unaowafahamu na uwaambie kuwa una muda wa ziada sasa hivi ambayo ungependa kuendesha abiria. Unaweza kukuta mmoja au hata zaidi katika watu unaowafahamu wakawa wana nafasi ya kukupa au wakawa wanafahamu mtu ambaye anaweza kukupa nafasi.
- Tafuta kazi mtandaoni: Zipo tovuti kama ZOOM Tz ambapo kuna ajira nyingi tu zinatangazwa mara kwa mara. Tembelea website na unaweza kukuta kazi ya dereva ambayo inaweza kuwa ni fursa nzuri sana kwa ajili ya kurudisha kipato chako.
Historia yako ya kuendesha abiria kwenye majukwaa ya programu za usafiri itakuwa ni nzuri sana katika kuonesha uzoefu wako kwenye CV yako. Kwahiyo uwezekano wa kutuma maombi na kupata ajira za udereva ni mzuri.
Mfano wa kampuni zinazokuwa na uhitaji wa madereva
- Usafiri wa sherehe: Watu wengi wana kampuni za usafiri kwa ajili ya sherehe. Hizi huhitaji madereva kwasababu ni biashara nzuri sana yenye uhakika wa wateja wa hadi kupitiliza. Na uzuri wa kazi hii ni kwamba unaweza kuifanya katika muda wa ziada huku ukiendelea kufanya shughuli sehemu nyingine. Unaweza kufahamu haya makampuni kwa kuulizia watu unaowafahamu. Kama kuna hata watu watatu ambao wanawafahamu watu waliokuwa na harusi wanaweza kukuulizia walipokodisha usafiri siku ya sherehe yao. Zaidi wanaweza hata kukupa mawasiliano ya walipokodosha usafiri huo.
- Usafiri wa misiba: Kampuni hizi zipo nyingi pia. Mara nyingi huwa na ofisi zao karibu na maeneo ya hospitali kubwa mfano Muhimbili. Majanga hutokea kila siku kwa hiyo biashara hii inatoa huduma sana. Tembelea ofisi na uulizie kama wanahitaji dereva wengine. Tena itakuwa vizuri zaidi kama utakuwa na business card yako ya kuwaachia. Hii itakufanya uonekane unafaa sana kwa hiyo ikitokea nafasi ni rahisi kuwasiliana na wewe.
- Usafirishaji wa mizigo/chakula: Kwa lugha iliyozoeleka hii ni delivery driving. Wapo wafanyabiashara wengi wanaohitaji madereva waaminifu kwa ajili ya kupeleka mizigo kwa wateja wao. Njia rahisi ya kuwapata ni kuingia instagram, kutafuta biashara na kuwatumia ujumbe kuwa unatoa huduma ya delivery. Mara nyingi hawa huwa ile ada yote ya delivery anapokea dereva bila kugawana tena na muuzaji. Hii inaweza kuwa nzuri zaidi kwa madereva pikipiki lakini kwa dereva wa gari pia kwasababu unaweza kukusanya mizigo mingi zaidi. Tembelea pia mahoteli yaliyopo karibu nawe na uwaachie business card yako ili wakipata order za delivery wawe wanakutafuta.
6. Endesha Taxi za kawaida
Unaweza kufata hatua maalumu za kufanya gari lako liwe taxi na ukaendelea na kuendesha abiria hata kama makampuni yote ya programu za safari yatasitisha huduma nchini.
Kama hauna gari basi unaweza tena kuwasiliana na watu wako wa karibu na kupata mtu mweye taxi au ambaye angependa kufanya gari lake liwe taxi.
Ili kupata mtazamo mzuri zaidi unaweza kutembelea kituo chochote cha taxi kilichopo karibu nawe na ukaweza kuongea na madereva kuhusu biashara hii.
Sekta ya usafiri wa Taxi za kawaida imeendelea kubaki ingawa programu za safari zimelivaa soko lake kwa kasi kubwa. Hii inamaanisha kuwa bado kuna fursa kwenye upande huu wa huduma ya usafiri. Kwa hiyo, unaweza ukafikiria kujaribu, hasa kwasababu upande huu hakuna hofu ya kwamba kampuni inaweza kusitisha huduma na fursa kutoweka.
7. Pata Updates kutoka Weibak
Tunafahamu kuwa mambo ni mengi na unaweza kupitiwa katika kufatilia vitu vinavyoendelea baada ya Uber kusitisha huduma Tanzania.
Sisi tupo hapa kwa ajili ya madereva, lengo letu kuwaletea taarifa sahihi za yanayojiri na jinsi ya kufanikiwa kwenye sekta hii ya usafiri kupitia programu za safari.
Tafadhali tuongezee mbinu nyingine katika comment ili madereva waliopoteza fursa baada ya Uber kusitisha huduma Tanzania waweze kupata kitu cha kuendelea
Kanusho: Weibak Carsharing sio mdau wa kampuni yoyote ya programu za usafiri. Lengo letu ni kusaidia madereva wa programu hizi kupata taarifa sahihi, kuwaunganisha na kuwaelimisha kuhusu jinsi ya kufanikiwa kwenye sekta hii kwa ujumla.
Rudini tufanye kazi wengine tumezoea kufanya kazi na Uber awa wengine miyeyusho tu atuwaelewi kabisa yani