faida za gari la kukodi

FAIDA ZA DEREVA KUTUMIA GARI LA KUKODI KUENDESHA ABIRIA

Kuanzisha biashara yenye faida kubwa kwenye programu za safari hakuhitaji kuwa na gari lako mwenyewe. Dereva anaweza kutengeneza kipato kwa kutumia gari la kukodi kwa mmiliki na kugawana naye sehemu ya mapato.

Katika makala hii utaenda kuona manufaa ya kufanya biashara hii ya usafirishaji abiria bila kuhitaji kununua gari. Kama tayari unao mtaji wa kununua gari kwa ajili ya biashara, utaenda kuona maoni yetu kama ni bora ununue gari au la.

FAIDA ZA KUENDESHA GARI LA KUKODI BADALA YA KUNUNUA LA KWAKO

1. HAUHITAJI MTAJI MKUBWA

Unapotaka kuanza biashara ya kuendesha abiria kwenye majukwaa ya programu za safari na tayari una gari la kukodi kwa makubaliano unakuwa ni kama umeanzisha biashara bila mtaji.

Kama umepata mmiliki mzuri wa gari basi utakuta tayari gari ipo kwenye hali nzuri na lina mafuta. Kwa hiyo wewe inakubidi tu kuliichukua na kuanza kazi. Yaani mtaji wako unakuwa ni muda wako pamoja na jitihada zako.

2. WEPESI WA KUANZA

Kabla ya kuanza biashara katika sekta ya usafiri wa taxi za mtandaoni, vipo vigezo vingi ambavyo mmiliki wa gari anatakiwa kuvifikia ili gari lake likubaliwe kuendesha abiria kwenye majukwaa husika.

Mfano wa vigezo hivi ni kuhakikisha wana kadi ya gari la biashara, kukata bima ya biashara, kufanya maboresho ya magari, kubadilisha plate namba kama bado ni za magari binafsi nk.

Haya yote dereva atayaepuka kama yeye anakodi gari kutoka kwa mtu. Mara nyingi wamiliki hukabidhi madereva magari ambayo tayari yameshatimiza kanuni zote za kubeba abiria.

Hii huhakikisha kuwa dereva anapata gari na kuanza kazi mara moja bila kuchelewa.

3. MALIPO YA KODI

Utakuwa tayari unafahamu kuwa magari yote ya biashara yanatakiwa kulipa kodi kwa mamlaka ya mapato kila baada ya muda uliokubaliwa.

Madereva wa kwenye programu za safari ambao wanamiliki magari yao hupeleka malipo yao kama kawaida. Lakini mara nyingi unapokodi gari, yule mmiliki wa gari ndiye mwenye jukumu la kulipa kodi ya biashara inayofanyika na chombo chake. Lakini hii pia sio mara zote kuna muda hutegemea na aina ya makubaliano yaliyopo kati ya dereva na mmiliki wa gari.

4. KUEPUKA GHARAMA ZA MATENGENEZO

Gari au chombo cha moto cha kukodi ni mali ya aliyenunua. Katika shughuli ya usafiri ambapo kila siku gari lipo barabarani upo uwezekano mkubwa sana wa hitilafu na ajali kutokea.

Yanapotokea haya mwenye gari ndiye anakuwa na jukumu la kutengeneza pale ambapo kweli tatizo halijasababishwa na dereva. Hii ni moja ya faida kubwa sana ya kutumia gari la kukodi kuendeshea abiria wa programu za safari.

Mara nyingi jukumu la dereva katika gari la kukodi ni kugharamikia vimiminika vya kwenye gari yaani mafuta pamoja na oil kama oil ya brake, ya usukani nk. Wapo wamiliki wengine wengi ambao hugharamia hata hizo oil na kumuachia dereva gharama za mafuta tu.

Lakini wapo madereva ambao wanasema kuwa wao hulipia mafuta pamoja na oil zote zitakazoisha wakati wa kuendesha abiria.

5. UWEZO WA KUBADILISHA MAGARI

Dereva anapoamua kutumia gari la kukodi kuendeshea abiria kwenye majukwaa ya usafiri wa mtandaoni anakuwa na uwezo wa kuchagua aina ya gari analotaka kuendesha.

Hii ni tofauti kidogo na unapokuwa na gari lako mwenyewe. Kwa mfano ukiwa unaendesha na aina ya gari ambalo labda ni dogo sana na abiria wengi hawatoshi vizuri, ni rahisi kutafuta mmiliki mwingine mwenye gari lenye nafasi kubwa zaidi na kuingia mkataba naye baada ya mkataba ulionao kuisha.

Pia magari aina fulani ambayo ni adimu zaidi kwenye majukwaa huwa yanapata wateja wengi zaidi. Kwa hiyo dereva anayeendesha magari ya mkataba na wamiliki huwa wepesi kugundua magari yepi yanapendwa zaidi. Hivyo wana uwezo zaidi wa kutafuta watu wenye aina hiyo ya magari na kuingia nao mkataba kuendesha na kugawana faida.

Faida nyingine ya uwezo wa kubadilisha magari ni pale ambapo gari linakuwa na matatizo mengi sana.

Kama gari lina hali mbaya na mmiliki anashindwa kulitengeneza basi ni rahisi kwa dereva kutafuta mkataba na mtu mwengine mwenye gari lenye hali nzuri zaidi.

Wakati kama wewe dereva ndiye mmiliki wa gari na gari lako ndio bovu na unashindwa kulitengeneza, unakuwa hauna budi zaidi ya kusimamisha biashara au kuendesha gari bovu na kutofurahisha abiria.

JE, KAMA UNA MTAJI WA KUTOSHA NI BORA KUNUNUA GARI AU KUINGIA MKATABA NA MTU MWENYE GARI?

Ili kujibu swali hili kwanza tuone faida za kuendesha gari unalomiliki mwenyewe

  1. FAIDA KUBWA ZAIDI: kama chombo ni cha kwako basi nauli yote unayopata inakuwa ya kwako. Hauna jukumu la kugawana na mtu yeyote zaidi ya kampuni za programu za safari.
  2. HAUNA BOSI: kwasababu wewe ndiye bosi. Baadhi ya madereva hupata wakati mgumu kutokana na misuguano katika mahusiano yao na wamiliki wa magari walioingia nao mikataba. Hasa kama wewe ni mtu unayependa kujipangia shughuli zako bila kufatiliwa sana, kumiliki gari lako kutakupa amani zaidi kuliko kuendesha la mtu mwingine.
  3. AMANI: Unapoendesha gari la mtu mwingine huwa kuna ile hofu ya kulipishwa pale matatizo yatakapotokea hata kwa bahati mbaya, au pale gari litakapoibiwa. Bila shaka pia janga litakalokuta gari la watu wewe ndio utakuwa mtuhumiwa wa kwanza. Lakini unapokuwa na gari lako hii hofu huwa haipo kabisa.
  4. MATUMIZI BINAFSI: Gari likiwa lako unaweza kuliendesha vyovyote unavyotaka hata kwa matumzi binafsi bila hofu yoyote

Baada ya kupitia faida hizi za kumiliki gari lako mwenyewe na faida za kuendesha gari la kukodi watu wengi hushauri kuanza na gari la kukodi kwanza.

Ukianza kwa kuendesha gari la mtu mwengine utaweza kufanya utafiti wa kina zaidi kuhusu biashara hii ya usafiri wa programu za safari na kugundua kama kweli itakuwa na faida ya kuweza kulipia gharama utakayoingia kununua gari kwa ajili ya biashara.

Mara nyingi usinunue tu gari kwasababu umesikia kuwa taxi mtandaoni zinalipa sana. Kwasababu ukweli ni kwamba kuna madereva wengine wanaona kama biashara hii hailipi. Lakini pia wapo wanaoona kwamba inawalipa, kwahiyo ni vizuri kujifanyia utafiti wako mwenyewe huku ukiendelea kutengeneza pesa.

Kwa hiyo ili kuepuka hasara ni vizuri kuanza kwanza kwa kuendesha gari la mtu mwengine upate ujuzi na uone faida. Ikikuridhisha ndio unaweza kununua gari lako.

Kama unataka tu kununua chombo cha usafiri kwa ajili yako binafsi na kufanya shughuli za usafiri kama ziada tu, unaweza kununua. Lakini kama dhumuni kuu la kununua gari ni biashara hii kwa kweli ni bora kusubiri na kuanza majaribio na gari la kukodi kwanza.

Wewe unaonaje juu ya hili? Kama unao mtaji kamili wa kununua gari utanunua kwa ajili ya kuendesha abiria wa programu za safari au utaanza kwanza kwa kutafuta gari la mtu wengine na kukusanya ujuzi na kufanya utafiti?

1 thought on “FAIDA ZA DEREVA KUTUMIA GARI LA KUKODI KUENDESHA ABIRIA”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *