Unapokuwa umeendesha abiria kwa muda mrefu kwenye majukwaa ya programu za safari lazima ifike wakati utathmini kama biashara yako inakuletea faida au la. Katika makala hii utaenda kuona dalili za hasara kwa madereva wa sekta hii, na pia tumekuchambulia suluhisho ili kuhakikisha unaendelea na biashara na kupata faida.
Ukweli ni kwamba wapo madereva wengi sana ambao wanafanya shughuli hii kwa muda mrefu bila kutambua kuwa mwisho wa siku wanatumika sana huku malipo madogo sana.
Hii haitakiwi kutokea kwako, hakuna mtu anayetakiwa kufanya biashara ya hasara hasa katika dunia hii ya leo na nchi kama hii ambapo uchumi unayumba kila kukicha.
DALILI ZA HASARA KWENYE BIASHARA YA TAXI MTANDAONI
1. GHARAMA YA JUU
Biashara yoyote haiwezi kufanikiwa kama vile gharama za uendeshaji wa biashara zinakuwa kubwa kuliko kipato kinachoingia. Zipo gharama nyingi ambazo madereva wa kwenye program za safari huingia kwasababu wao ni watoa huduma binafsi na sio waajiriwa wa makampuni haya ya usafiri.
Mfano wa gharama ni kama ifuatavyo:
- Mafuta ya gari
- Matengenezo gereji
- Usafi wa gari (Car wash)
- Oil au vilainishi vya gari
- Chakula na vinywaji kwa ajili ya dereva
Hizi ni baadhi tu ya gharama ambazo huwa zinajirudia rudia katika biashara hii ya taxi mtandaoni.
Madereva wengi hata hawafuatilii sana gharama hizi katika kuangalia kama kweli biashara ina faida au la. Au kama faida ipo ni ya kiasi kinachofaa kuendelea na biashara au ni kodogo sana.
Ukiongezea pia kuwa bei ya mafuta ihupanda na kushuka huku bei ya nauli inakuwa palepale, uwezekano wa kufanya biashara ya hasara ni mkubwa. Kwa hiyo umakini mkubwa unahitajika ili kuhakikisha gharama inadhibitiwa vya kutosha kwa ajili ya kuepusha hasara.
SOMA: JINSI YA KUOKOA GHARAMA YA MAFUTA YA GARI
2. FAIDA NDOGO
Vitu viwili vinavyotumika kuhesabu faida ni matumizi na mapato. Ili faida iwe kubwa dereva anatakiwa awe aidha ana matumizi madogo au awe anapata safari nyingi zaidi.
Kama vile wewe matumizi yako ni madogo lakini bado faida ni ndogo, inamaanisha kuwa haupati safari za kutosha. AU unaweza kuwa unapata safari za kutosha lakini nauli ikawa ndogo sana.
Siku zote iashauriwa madereva kuwa makini sana katika mahesabu ili kujua mapema kama biashara inalipa na kuepusha kupoteza muda.
3. MASAA MENGI KAZINI
Kutokana na sheria za kazi, mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi masaa 8, ikizidi sana 10. Wapo watu wengi ambao hufanya kazi kwa masaa haya na hutengeneza kipato kizuri tu.
Mara nyingi madereva wa programu za safari hufanya kazi zao kwa masaa mengi sana kwa siku kwasababu ndio jinsi ya kuongeza uwezekano wa kutengeneza pesa zaidi.
Lakini inapofikia sehemu ukajikuta unafanya kazi masaa mengi sana kwa siku hadi kufikia kutopata muda wa kutosha wa kupumzika ujue kuna tatizo.
Mtu anayepata kipato cha kutosha mara nyingi huweza kujipatia muda wa kupumzika. Watu wanaokuwa na uhitaji mkubwa sana wa faida hujikuta wakilazimika kuwa hewani hata kama wamechoka sana.
Kwa hiyo utakapoona kuwa unaanza kujilazimu kuendesha abiria kwa masaa mengi sana inabidi kujitathmini uone kama faida ipo au unafanya kazi sana kwasababu umeona kuwa faida ni ndogo.
4. KUTOSIKILIZWA NA UONGOZI
Unapokuwa unafanya kazi kwenye kampuni yoyote ambayo haiwapi kipaumbele watoa huduma ujue hasara ipo mlangoni.
Hii ni kwasababu malalamiko huwa hayasikilizwi na kufanyiwa kazi mapema. Mfano kama madereva wanalalamika nauli ni ndogo, hadi wasikilizwe na nauli ibadilishwe watakuwa wameshapata hasara kiasi gani?
Tukiangalia pia tatizo kama la madereva kukatwa nauli kwa asilimia kubwa. Suala hili limelalamikiwa kwa miaka mingi bila kufanyiwa kazi mpaka LATRA ilipoingilia kati na kuweka sheria za makato.
Hii inaamaana madereva miaka hii yote wamepata hasara kiasi gani?
Kwahiyo kutosikilizwa mapema ni moja ya dalili za hasara kwa madereva ambayo hata sisi tunatamani makampuni ya programu za safari yaweze kuifanyia kazi.
5. MALALAMIKO KUTOKA KWA MADEREVA WENGINE
Kama unaendesha abiria kwenye jukwaa fulani na ukagundua kuwa madereva wengine kwanza wana malalamiko mengi au wana malalamiko kama ya kwako ujue kuna tatizo.
Kampuni zenye malalamiko sana maana yake ni kwamba zina historia ya kutosikiliza madereva. Hatusemi kwamba ukatishwe tamaa na masimulizi ya majanga ya watu wengine.
Tunachosema ni kwamba ukae chonjo maana mara nyingi madereva hulalamika pale wanapoona biashara kama inawanyonya na hawapati faida. Watu wanaopata faida vizuri huwa hawalalamiki na mara nyingi huvumilia mengi chini kwa chini.
Ukiona kelele nyingi sana ujue kuna hasara ambazo madereva wanapata.
6. MATATIZO KUJIRUDIA RUDIA
Unapokuwa unaendesha abiria wa jukwaa fulani la programu za safari na ukagundua kuwa miaka nenda miaka rudi matatizo yanajirudia rudia uchukue hilo kama dalili ya hasara.
Kwa mfano kampuni ambayo mara nyingi hawalipi madereva fidia ya kufata abiria aliye mbali. Au yale ambayo yanafunga akaunti za madereva mara kwa mara bila kuchunguza kiundani. Au jukwaa linalopata hitilafu mara kwa mara.
Kama matatizo unayopitia kwenye biashara yanajirudia rudia au hayasuluhishwi ujue lazima kuna hasara utaipata.
7. MWAMKO WA BIASHARA KUSHUKA
Mara nyingi madereva wanapoanza kazi ya kuendesha abiria kwenye programu za safari huwa na mori ya kufanya kazi nzuri na kutengeneza kipato kiuhalali kabisa.
Dereva unapojigundua kuwa ile mori ya kazi imeshuka au imeondoka kabisa ujue kuna dalili kuwa hautafanya kazi kiufanishi hivyo kushusha faida.
Hii haimaanishi kwamba kosa la kushuka mori ni lako kwasababu, madereva hupitia changamoto nyingi sana katika biashara hii ambazo huweza kuondoa kabisa hamu ya kazi hata kuleta hasira kwa mtu yeyote yule.
Mara nyingi watu wanaopata faida nzuri huwa siku zote wana mori ya kufanya kazi. Ila wale ambao wanapata hasara huwa wanakatika moyo.
8. MSONGO WA MAWAZO
Pesa ni muhimu ndio lakini, pale chanzo chako cha pesa kinapokupa stress basi bila shaka utajikuta unapata hasara mwisho wa siku.
Kwa muda mrefu sana madereva wengi wa programu za safari wamekuwa wakipitia changamoto ambazo zinawasumbua akili.
Haya matatizo ya kila kukicha huweza kupelekea utendaji wa kazi kushuka na hata kuathiri afya ya mwili. Utendaji kazi unaposhuka katika kazi ambayo tayari kwa mtazamo wa baadhi ya watu ina mapungufu kama hii hasara haiwezi kukosekana.
9. GARI KUSHUKA UBORA
Katika kupanga nauli na makato haieleweki kama kampuni zilizingatia kuhusu suala la magari ya madereva kushuka ubora kutokana na kuendeshwa mara kwa mara katika kutoa huduma.
Kama dereva anatumia gari lile lile baada ya muda lazima ubora wake utashuka kwasababu litakuwa imesafiri kilomita nyingi sana.
Gari linaposhuka ubora huku nauli ipo pale pale na makato bado yanaonekana makubwa, ni lazima kuna kiasi fulani cha hasara ambacho dereva au mmiliki wa gari huingia bila hata kujijua.
Kwa hiyo kama dereva umekuwa ukiendesha abiria kwenye majukwaa kwa muda mrefu na ukagundua kuwa gari lako unaloendesha limeanza au limeongezeka uchakavu ujue hiyo ni hasara unaingia.
Hii ni kwasababu itakubidi ukate tena hela kwenye faida unayopata ili kurudisha gari kwenye ubora wake wa zamani au ili kuongeza ubora kidogo.
SULUHISHO
Ukishagundua dalili za hasara kwenye biashara yako unaweza kuchukua hatua zifuatazo ili aidha kuondoa hasara kabisa au kupunguza:
- Rekodi gharama zote na mapato yote: Hii itakusaidia kuona kama kweli kuna hasara unapata au kama faida ipo ni kiasi gani.
- Badili gari: Kama unaendesha gari linalotumia mafuta sana, angalia uwezekano wa kubadilisha au unaweza kufunga mfumo wa gesi na kuokoa gharama ya mafuta. Kama wewe unaendesha gari la mtu mwengine ambalo linakuingizia gharama kubwa basi fikiria jinsi ya kupata gari tofauti baada ya mkataba kuisha.
- Badili jukwaa: Yapo makampuni mengi ya programu za safari Tanzania na mengine yanaendelewa kuzaliwa. Kama jukwaa ulilopo linakutia hasara basi usisite kujaribu lingine.
- Wasikilize madereva wengine: Jiunge kwenye vyama au ma group ya madereva taxi za mtandaoni na uwasikie wao wanazishindaje changamoto na kutengeneza faida. Madereva wengi sana ni wema sana na wanapenda kushirikisha wenzao.
- Dondoo kutoka Weibak Carsharing: sisi tupo hapa kwa ajili ya madereva, hatuna ubia na kampuni yoyote ile ya hizi programu za safari. Lengo letu ni kufanya tafiti kwenye sekta hii na kuwapa elimu yetu madereva wa programu za safari ili waweze kufanikiwa katika fursa hii kama madereva wa nchi za nje wanavyofanikiwa.
Je umegundua dalili za hasara kwenye shughuli yako ya kusafirisha abiria wa majukwaa ya safari? Ni hatua gani umechukua kuhakikisha kuwa unapata faida ya kutosha?
Tafadhali sana tushirikishe kwenye sehemu ya comments. Pia usisite ku share makala hii kwa madereva wengine ili na wao waweze kupata chochote kupitia wewe.
Hata sisi madereva wa bolt hatupati faida zaidi ya asara unafanya kazi ya sh 70000 kulipa Deni 15000 je mnamsahada upi kwa upande wenu
Aaww kazi ya taxi ya mtandaon ni utumwa kwasbabu ya ufinyu wa elimi ya uelewa ya madereva
Bwana nyie ni bolt mnatuzuga tu hapa