Changamoto za Uber, Bolt Fursa kwa Majukwaa Mengine ya Teksi Mtandao?

Ni majira ya saa mbili asubuhi katika jiji la Dar es Salaam. Nikiwa ofisini, nakumbuka kuwa siku hii niliweka miadi ya kufanya mahojiano na Katibu Mkuu wa chama fulani. Bila kupoteza wakati, nachukua Kamera na vifaa vingine vitakavyoniwezesha kufanya mahojiano na kurekodi.

Kama ilivyo desturi, nachukua simu na kuwasha programu ya Bolt kwa ajili ya ‘ku-request’ gari. Ilikuwa ni lazima ‘ni-request’ gari kwa sababu nilibeba vifaa vya gharama na vinavyohitaji kubebwa kwa umakini mkubwa. Wakati nikihangaika ‘ku-request’ gari, nagundua kuwa huduma ya magari haipo kwa sasa. Muda umenitupa mkono, nahitaji kuwahi. Ikanilazimu ‘ku-request’ Bajaji (ya matairi matatu), nikaianza safari kuelekea kule alipo katibu mkuu wa chama.

Nikiwa njiani, kila wakati nililazimika kufuta vumbi lililokuwa likitimkia ndani ya Bajaji na kunasa kwenye Kamera ambayo nilikuwa nimeishika mkononi. Hii ndio hali niliyokuwa nikijaribu kuikwepa tangu awali kwa kutaka huduma ya gari, kwani kama ningepata huduma ya gari ningepata mazingira rafiki kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vyangu. Hali hii ilinifanya kutoifurahia kabisa safari yangu.

Niliendelea na zoezi hilo la kufuta vumbi linalonasa kwenye Kamera kila mara tulipopita barabara zinazofanyiwa matengenezo mpaka tulipofika mwisho wa safari yetu.

Baada ya muda wa masaa takribani mawili, tukawa tayari tumemaliza kufanya mahojiano yetu. Na sasa ulikuwa ni muda wa kufungasha vifaa vyangu tayari kwa kuanza safari ya kurejea ofisini. Kwa wakati huu nilihitaji ‘ku-request’ usafiri wa kunirejesha ofisini. Sikutamani tena kutumia bajaji kurudi ofisini kutokana na changamoto nilizozipitia wakati nakuja kwenye mahojiano. Yale mawazo ya kufuta vumbi kwenye Kamera njia nzima yalinipelekea kufikiria kujaribu kutumia majukwaa mengine ya taksi mtandao ambayo yanatoa huduma za usafiri wa gari.

Fursa kwa majukwaa mengine ya taksi mtandao?

“Ikiwa Bolt hawatoi tena huduma ya usafiri wa magari, inabidi nijaribu programu mpya kuona kama nitapata gari” nilijisemea. Baada ya kupitia programu kama tatu hivi, hatimaye macho yangu yakatua kwenye programu ya Paisha, maelezo yake yakanipa shauku iliyonisukuma kuisakinisha programu hii kwenye simu yangu. Baada ya dakika kama tatu hivi, Paisha tayari ikawa inapaa kwenye simu yangu.

Bila kupoteza wakati nikatafuta huduma ya usafiri wa gari na hatimaye nikaipata. Ilichukua dakika kama tano hivi kwa gari nililo ‘request’ kufika mahali nilipokuwepo kwa ajili ya kunichukua na kunirejesha ofisini kwangu.

Tukiwa njiani, dereva anapokea simu ambayo kutokana na mazungumzo yake iliashiria kuwa alikuwa anaongea na dereva mwingine ambaye naye anatoa huduma ya usafiri kupitia majukwaa ya taksi mtandao.

Katika mazungumzo yao, dereva huyu akawa anamwelezea dereva mwenzake jinsi ambavyo amekuwa akijaribu kutumia majukwaa kadhaa kutoa huduma ya usafiri wa gari baada ya huduma hiyo kutolewa katika jukwaa la Bolt.

“Sasa hivi niko Paisha. Ninapaa tuu. Wale wamezingua lakini mwisho wa siku lazima Maisha yaendelee”. Alisema dereva huyu kumjibu yule aliyekuwa akiongea nae kupitia simu.

Kutokana na mazungumzo yale, nikapata shauku ya kumdadisi kwa maswali kadhaa ambayo yaliibuka kichwani kwangu kutokana na kusikiliza mazungumzo yake katika simu.

Nikafungua mazungumzo yetu kwa kumuuliza swali “Una muda gani toka umeanza kutumia Paisha?”. Dereva akanijibu ‘Nina kama wiki mbili hivi, lakini kabla ya hapo nilikua natumia Bolt”.

Majibu yake yakanipeleka moja kwa moja kwenye swali la “Kwa nini umeacha kutumia Bolt?”. Dereva huyu bila kusita akanijibu “Bolt kufunga huduma ya gari kwa watu binafsi ni hasara kwangu, na mwisho wa siku ni lazima maisha yaendelee. Walipositisha huduma ya gari ikanilazimu kujaribu kutumia programu nyingine na nikapendezwa zaidi na Paisha”.

Mpaka nafika ofisini, tayari nilikuwa nimepata majibu ya maswali yangu kutoka kwa dereva wa Paisha. Wakati naingia ofisini nikawa najiuliza “Ni abiria wangapi waliopata changamoto kama nilizopitia mimi hata kupelekea kujaribu kutumia majukwaa mengine ya taksi mtandao? Na ni madereva wangapi wamepitia changamoto kama alizopitia dereva huyu hata kuwapelekea kuanza kutumia majukwaa mengine kutoa huduma ya taksi mtandao?

Maswali haya yakanirejesha moja kwa moja katika mazungumzo yangu na dereva wa Paisha, aligusia kuwa wakati anaanza kutumia Paisha kutoa huduma ya taksi mtandao hakukuwa na wateja wengi, lakini kadri siku zinavyokwenda amekuwa akipata ‘requests’ nyingi ikilinganishwa na awali, ikiashiria kuwa abiria pia wanazidi kuongezeka kila siku.

Ni dhahiri kuwa mimi niliacha kutumia Bolt kutokana na kukosa huduma ya usafiri wa gari. Halikadhalika kwa dereva wa Paisha, yeye aliacha kutumia Bolt kutokana na kukosa wateja wanaohitaji usafiri wa gari. Hivyo ikamlazimu kutumia jukwaa tofauti na Bolt kuendelea kutoa huduma. Wakati Uber imesitisha huduma zake nchini, na Bolt kusitisha huduma za usafiri wa gari kwa abiria binafsi, abiria pamoja na madereva wanajaribu kutumia majukwaa mengine ili kupata huduma ambazo wamezikosa kutokana na changamoto walizonazo Uber na Bolt. Bila shaka, hii ni fursa kwa majukwaa mengine kupata ‘spotlight’ na kuzingatiwa sokoni.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *