Baada ya maamuzi ya ada mpya ya programu za safari kuwa 15% kutangazwa 16 Aprili 2022. Na baada ya kampuni kubwa na kongwe ya Uber kusitisha huduma kutokana na mabadiliko haya, wadau wengi wamekuwa wakisikilizia kama Bolt itabaki au itasitisha huduma pia.
Tangu agizo la kamisheni mpya kutolewa na LATRA, kampuni ya Bolt iliamua kuheshimu na kuendelea kutoa huduma. Lakini ilitoa taarifa kwamba imechukua hatua hii kwa shingo upande kwasababu 15% ni ndogo kwa kuendesha biashara.
Mara baada ya tamko rasmi kutoka LATRA, Meneja wa Bolt kanda ya Afrika Mashariki, Kenneth Micah alisema kuwa Bolt iliomba kukutana na wadau husika ili kujadili zaidi suala hili kwa matumaini ya kufikia muafaka wa kanuni nzuri za ushuru na kamisheni, huku ikiendelea kutafuta njia mbadala zilizomo ndani ya mfumo wa kisheria na mfumo wa udhibiti wa Latra.
Kampuni ya Bolt ambayo ilikuwa inatoza 20% kwa ajili ya ada kwa madereva ilisema kuwa, itabidi kuondoa huduma za za usafiri wa magari na kuacha vyombo vingine tu viendeshe abiria kwasababu ada ya 15% si rafiki kwa kuendeshea biashara katika soko hili.
Amuzi hili pamoja na amuzi la kampuni ya Uber kusitisha huduma yangemaanisha kuwa makampuni madogo na mapya kama ping, Linkee, Moovn nk yangekuwa yanaachiwa soko kubwa sana kutoka kwa magwiji hawa wawili.
Meneja wa Bolt aliendelea kusema kuwa “Wakati tunakubali na kuthamini mamlaka ya Latra, tunaamini kwa dhati kwamba kuanzishwa kwa sheria wa udhibiti katika sekta inayofanya vizuri na yenye ushindani ni hatari kwa uchumi wa soko huria. Hata hivyo, Bolt imetekeleza agizo hilo kwa kulazimishwa ila ni kwa muda tu”.
Kampuni ya Bolt itabaki au itasitisha huduma ya usafiri?
Wiki 3 zilizopita meneja wa Bolt alinukuliwa zaidi wakati akiongea na waandishi kuwa “Tunatii kwa muda ili kuonyesha nia njema na kujitolea kwetu kushirikiana na Latra kwa kanuni zinazofaa zaidi na zinazowezesha uwekezaji zaidi. Tunafahamu ukweli kwamba iwapo Latra itadumisha hali ilivyo sasa, soko hatimaye litakoma kuwa na faida kwa Bolt, na hii italazimu kuzima kitengo chetu cha magari.”
Hii ilionesha kuwa kuna dalili nzuri ya kampuni hii kuendelea kutoa huduma kwasababu kama wangetaka kusitisha wangesitisha kama Uber.
Kwasababu kampuni ilitoa tamko kuwa inaendelea kujadiliana na wawekezaji pamoja na Latra, inaonekana kuwa wana imani kuwa muafaka unaofaa utaweza kufikiwa.
Bolt imeamua kuendeleza huduma
Mapema mwezi huu kampuni ya Bolt imetoa taarifa maalumu kuhusu maamuzi yake ya kuendelea na huduma. Kufuatia kufanikiwa kukaa kikao na Latra kampuni imeamua kutengua maamuzi yake ya kuondoa huduma zake. Pia inaendelea majadiliano na Latra na inategemea mabadiliko sahihi yataendelea kutekelezwa.
Meneja wa Bolt kanda ya Afrika Mashariki amenukuliwa kwenye gazeti la Daily news la tarehe 06 May 2022 akisema, “Kutokana na kikao tulichofanya tungependa kuwaarifu kuwa tumepiga hatua kubwa katika kutatua suala hili na tutategemea suluhu ya haraka”
Aliendelea pia kwa kusema ” Bolt inapenda kusisitiza kwamba imejitolea kuendelea na huduma katika soko la Tanzania na kutengeneza fursa za ujasiriamali zitakazowawezesha watu wengi zaidi kujikimu kimaisha.”
Sababu za kampuni ya Bolt kutositisha huduma Tanzania kama Uber
A. Latra kufanya mapitio ya tamko la kwanza
Kama ambavyo meneja alivyoahidi, kampuni ilifanikiwa kukutana na Latra kuzungumza juu ya kuleta unafuu kwa makampuni ya programu za safari hasa katika upande wa ada ya huduma za jukwaa kwa madereva.
Kutokana na vikao mbali mbali Latra iliamua kufanya mabadiliko katika vipengele vitatu kama ifuatavyo.
- Umbali wa juu zaidi kwa kilomita
- Kiwango cha kamisheni (ada anayokatwa dereva)
- Kiwango cha bei kwa kilomita (kimepandishwa kutoka 450tsh/km hadi 900 tsh/km kwasababu ya bei ya mafuta kupanda)
Kampuni imepata moyo na uhakika kuwa mabadiliko sahihi yanakuja hivyo hakuna sababu ya kusitisha biashara.
B. Uber kusitisha huduma Tanzania
Mwisho wa siku hii ni biashara na pale mtawala mkubwa wa soko anapoondoka basi mpiganaji anayefuata hupata nafasi kubwa zaidi ya kufanya biashara kubwa.
Ingawa zipo kampuni nyingi sana za programu za safari Tanzania, Bolt inachukua nafasi ya pili katika kuwa na watumiaji wengi zaidi.
Madereva wengi wa Uber huendesha Bolt pia. Kwa hiyo kusimama kwa Uber lazima kutakuwa kumesababisha kwa kiasi fulani madereva wengi na abiria pia kuhamia kwenye kampuni ya Bolt.
Kampuni ya Bolt nayo ingesitisha huduma basi ingekuwa bahati kubwa sana kwa makampuni madogo na mapya ya kwenye sekta hii.
Je Kama Latra haitafanya mabadiliko mazuri kampuni ya Bolt itabaki au itasitisha huduma?
Ingawa Mamlaka imeonesha kufikia maamuzi mazuri na kampuni hii, inaweza kutokea kwamba utekelezaji ushindikane kufikia viwango ambavyo Bolt inapendelea.
Hii ni kwasababu sekta hii ya programu za safari bado inakua, kwa hiyo udhibiti wake unaweza kubadilika kwa sababu ya maboresho.
Ikitokea hivi basi mambo mawili yanaweza kutokea kama ifuatavyo:
A. Bolt kusimamisha huduma:
Hii ni kwasababu hakuna biashara inayoweza kuendelea kama faida haikidhi uendeshaji. Kama kiwango cha kamisheni au bei za nauli kitakuwa chini sana basi kampuni itakuwa haina budi bali kukata tamaa na kuendelea tu na nchi zenye faida.
B. Bolt kuendelea na huduma:
Kutokana na kampuni ya Uber kusitisha huduma, Bolt ina nafasi kubwa zaidi ya kupata abiria zaidi na madereva zaidi. Hii itamaanisha kuongezeka kwa kipato kwa mwaka huu wa mabadiliko.
Kama wataalamu wataona kuwa ongezeko hili litafidia ile hasara ya kupunguzwa kamisheni na kupelekea kuongezeka faida sana, basi kampuni lazima itaendelea tu.
Je mtazamo wako ni upi? unaona kampuni hii itaendelea vizuri na kuchukua nafasi ya kwanza iliyoachwa na Uber au na yenyewe itaondoa huduma?
Sioni sababu ya Latra kufanya makubaliano mapya na Hawa mabeberu wa Bolt na Uber .Kwa miaka mingi sana toka kuanzishwa huduma zao hapa Tanzania wamekuwa wakiwanyonya madereva na wamiliki wa magari na kusababisha maisha duni kwa madereva na wawekezaji(wamiliki)wa magari .Mapendekezo yaliyotolewa na Latra ikiwemo ada ya 15%kwa safari na Bei ya tsh900/km yanapaswa kuendelea.Kama wao wanaona Biashara haiwalipi simple tu wafunge Biashara.
Hebu tujiulize swali moja ni vipi wamiliki wa Daladala na Mabasi ya mikoani ambao wanamiliki vyombo hivo ,wakifanya service,kununua spares na kulipa madereva mishahara ,kulipa Kodi za serikali wao wawe tayari kutoa huduma kwa kwa Bei elekezi ya Serikali .Halafu wanatokea madalali Fulani ambao mimi nawaita wezi hawa Bolt na Uber ambao hawamiliki chochote zaidi ya app zao ,hawafanyi service na hawalipi madereva ,wa kununua spares .Eti wakatae Bei elekezi za serikali yetu tukufu.Hii ni dharau kubwa sana kwa nchi yetu.Naomba serikali(Latra)isirudi nyuma ,hawataki kutii Bei elekezi waende ziko kampuni zitakuja na kufanya kazi na waTanzania kwa mafaa yao na waTanzania kwa ujumla.
Naomba kuwasilisha.