BOLT IMEONGEZEWA UFADHILI

BOLT IMEONGEZEWA UFADHILI WA TRILIONI 1.5

Kuanzia tarehe 11 Januari 2022 Kampuni ya Kiestonia ya Bolt imeongezewa ufadhili wa Euro milioni 628 sawa na shilingi za kitanzania Trilioni moja, bilioni mia tano themanini, milioni mia moja sabini, laki tatu elfu nne mia nane themanini na nne.

Kampuni hii imekuwa ikihitaji fedha hizi kwasababu ya mipango mikubwa ya uboreshaji huduma ambayo imepanga katika nchi zote zenye huduma za Bolt.

Kwa miaka mingi tangu ianzishwe, kampuni ya Bolt imekuwa mpinzani au mshindani mkubwa wa Kampuni kubwa duniani ya usafiri wa ride hailing (Uber). Kwa hiyo mtaji huu uliopatikana bila shaka utaenda kusaidia kampuni ya Bolt iweze kuteka zaidi soko la ride hailing.

DHAMIRA YA KAMPUNI YA BOLT

1. KUPUNGUZA UHITAJI WA KILA MTU KUWA NA GARI

Kampuni ya Bolt imejikita sana katika kusaidia kupunguza athari za moshi wa magari (kaboni) katika layer ya Ozoni. Siku zinavyozidi kwenda ndivyo magari yavyozidi kutoa moshi ambao una madhara kwa viumbe hai pia kwa ubora wa hewa safi duniani.

Tatizo la global warming au ongezeko la joto duniani linafahamika kusababishwa na kaboni kuharibu layer ya ozoni ambayo ndio inayokinga dunia na malie mikali ya jua yenye athari kubwa sana.

Kwa hiyo Kampuni ya bolt ina ndoto au lengo la kutoa huduma ya usafiri huku ikipunguza kiasi cha kaboni kutoka kwenye magari.

2. KUPUNGUZA KERO YA UHABA WA MAEGESHO YA GARI

Kampuni ya Bolt imetambua kuwa miji mingi mikubwa ina tatizo la upungufu wa sehemu za kuegesha magari hasa kwenye maeneo muhimu. Kutokana na hili imekuwa ikiendelea kukusanya mtaji au ufadhili ili kuweza kuwekeza kwenye maeneo mazuri mijini ya kupaki magari ya Bolt kirahisi.

Pia itatimiza lengo hili kwa kutanua huduma za Bolt ili kufanya watu wengi watumie Bolt badala ya kwenda makazini au mikutanoni na magari yao ambayo yataishia kuchukua nafasi kubwa kwa kuegeshwa siku nzima mjini.

Hii itasaidia sana kupunguza msongamano na kupunguza pia kiasi cha magari barabarani yanayotoa moshi mbaya kwa mazingira.

3. KUONGEZA MATUMIZI YA MIBADALA YA GARI

Bolt ina lengo la kusaidia kila mji wenye huduma zake uwe na uwezo wa kusafirisha abiria kwa njia nyingine kama baiskeli za kielektroniki na bajaji za umeme ili kupunguza moshi.

Pia ina lengo la kupunguza safari za watu kwenda mjini kununua bidhaa kwa kupitia huduma za kuletewa mtu alipo au delivery.

Katika nchi za Afrika Bolt green program imekuwa ikisisitiza madereva kutumia magari yanayotumia gesi asilia au CNG ili kupunguza moshi wa mafuta kama petroli.

Kwasababu bado nchi yetu haijaendelea sana kimiundo mbinu na hatuwezi kutumia baiskeli za kielektroniki kwa wingi. Angalau njia hii ya kutumia gesi asilia badala ya petroli itasaidia sana kupunguza utengenezwaji wa kaboni na kutunza mazingira yetu.

4. KUPUNGUZA MSONGAMANO

kampuni ya Bolt ina lengo la kusaidia miji kuwa salama zaidi na ya kuvutia zaidi kwa kupunguza msongamano wa magari. Hili litatimia pale wakazi watakapogundua kuwa ni nafuu zaidi kupanda Bolt kuliko kuendesha magari yao binafsi.

Jambo hili litasaidia sana kupunguza kiasi cha magari barabarani na kupelekea kupungua kwa tatizo la foleni ambalo limekuwa likitusumbua kwa miaka mingi sana.

Pia kupungua kwa msongamanowa magari barabarani kutaongeza usalama kwa watembea kwa miguu na watumiaji baiskeli.

KWANINI KAMPUNI YA BOLT IMEONGEZEWA UFADHILI?

Hii ni kwasababu kampuni ina dhamira nzuri (kama ya kuendeleza miji na kulinda mazingira) ambazo zinakubaliwa na wawekezaji wakubwa duniani. Pia kwasababu kampuni imekuwa ikikua vizuri kifaida ingawa inashindania soko na kampuni kubwa sana ya Uber.

Wawekezaji wengi wakubwa duniani huwa hawatoi tu hela zao na kuwekeza kwenye makampuni ambayo hawana uhakika nayo kimafanikio.

HII INA MAANISHA NINI KWA MADEREVA WA BOLT TANZANIA?

KWANZA: kabisa kama ambavyo tumesema, kampuni imepata uwekezaji mkubwa hivi kwasababu imekuwa ikiingiza faida na hawa wawekezaji wana uhakika kwa kiasi kikubwa kuwa kampuni itaendelea kukua na kuleta faida nyingi zaidi.

PILI: Sehemu ya hizi fedha itaenda kutumika katika uboreshaji wa huduma kwa abiria lakini pia kwa madereva. Hii ni kwasababu madereva ndio kila kitu katika utengenezwaji wa faida kwa makampuni haya.

TATU: Bolt imeongezewa ufadhili kwasababu inataka sio tu kuboresha bali kutanua wigo wa huduma zao. Hii inamaana huduma ambazo tayari madereva wanafaidika nazo nchi za nje zitaanza kuzinduliwa kwenye nchi hizi zetu ambazo hazijaanza. Pia huduma mpya nazo zitaanza kama alivyosema Markus Villig mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Bolt.

Kwa hiyo sasa madereva watakapokuwa wanatoa malamiko itakuwa rahisi kwa kampuni kufanyia kazi malalamiko hayo.

“Kwa miongo kadhaa, miji imejengwa kwa magari ya kibinafsi, badala ya watu wanaoishi na kufanya kazi ndani yake. Huku Bolt, tunadhani mbinu hii imepitwa na wakati, ndiyo maana dhamira yetu ni kuunda miji kwa ajili ya watu, si magari

Markus Villig, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji, Bolt

Sisi hapa Weibak Carsharing tunafahamu sana kuwa kampuni ya Bolt imekuwa na malalamiko mengi zaidi ya makampuni mengine ya ride hailing hapa Tanzania

Madereva wanalalamika changamoto nyingi, masuluhisho hayaonekani, huku abiria wanalalamika zaidi kuhusu ubora wa chini wa huduma.

Abiria kero zao huwa wanasikilizwa kiurahisi kwasababu wao wanatoa hela na ndio wanathaminiwa zaidi. Ndio maana hata sasa ukienda kwenye kurasa za mitandao ya jamii za Bolt utakuta lawama 95% ni kutoka kwa abiria na ndio wanasikilizwa zaidi.

Madereva wengi hawana pa kukimbilia na kusikilizwa inapokuja kwenye suala zima la changamoto zao. Ndio maana sisi tumeleta uwanja huu wa Weibak Carsharing ili madereva nao waweze kusema changamoto zao, kupata dondoo na njia za kutatua changamoto hizo na kutengeneza faida zaidi.

Kwasababu Bolt imeshaongezewa ufadhili, sisi tutaendelea kufatilia ili kuona kama kampuni itafanya mabadiliko yoyote yenye kunufaisha madereva.

Kwetu sisi tunapenda madereva waweze kufanya kazi katika majukwaa haya ya ride hailing kwa ufanisi na bila kero ili waweze kufanikiwa.

Matumaini yapo kwasababu fedha zilizopatikana ni nyingi. Na siku zote kampuni ikipata mtaji mkubwa kama hivi huwa inafanya maboresho ambayo yanafarijisha.

Kwa hiyo endelea kufanya kazi Bolt, endelea kutoa huduma bora na kuwa wa kipekee na si kama wale madereva ambao abiria wanawalalamikia kila kukicha.

Pia kwenye sehemu ya comment tushirikishe mawazo yako juu ya taarifa hii. Unadhani kuwa hali itaenda kubadilika na kuwa nzuri kwa madereva au?

1 thought on “BOLT IMEONGEZEWA UFADHILI WA TRILIONI 1.5”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *